Utamu wa ndizi nyama zilizopikwa kwenye jiko la umeme

Na Mariam John
9 Jul 2022
Zinaiva haraka na kukupatia ladha ya kipekee wakati wa kula.
article
 • Kwanza zinaiva haraka na kukupatia ladha ya kipekee.
 • Hakikisha umeandaa ndizi, nyama, viazi mviringo, kitunguu maji, karoti, hoho, chumvi na mafuta ya kupikia.

Je, unatumia nishati gani ya kupikia ndizi nyama nyumbani kwako?

Kumekuwa na mitazamo tofauti ya kupika chakula kwenye umeme, wapo wanaosema kinapoteza radha na wapo wanaodai umeme unatumika mwingi.

Wapo wanaoogopa kuwa linaweza kusababisha shoti, hivyo kulazimika kutumia aina nyingine za nishati.

Pamoja na mitazamo yote hiyo, leo tutatumia dakika 35 kuandaa chakula chetu cha ndizi nyama na kitakuwa tayari kwa kuliwa. 

Mahitaji

Ili kupika chakula hiki tunatakiwa kuwa:

 1. Ndizi mshare 10 
 2. Viazi mviringo vinne
 3. Kitunguu maji kimoja
 4. Karoti moja
 5. Hoho moja 
 6. Chumvi na maji vikombe vitat
 7. Mafuta ya kupikia kijiko kikubwa kimoja
 8. Tangawizi nusu kijiko, 
 9. Nyama ya ng’ombe ½ kilo na tui la nazi kikombe kimoja

Twende jikoni

Osha nyama kisha katakata kulingana na vipande vya ukubwa unaopendelea, changanya nyama, chumvi na tangawizi iliyopondwa. Ongeza vikombe viwili vya maji kisha bandika kwenye sufuria maalum la kupikia kwenye jiko la umeme na uache kwa muda wa dakika 20.

Wakati nyama ikiiva, paka mikono yako mafuta kidogo ya kupikia kisha menya ndizi na viazi, vikate na uviweke kwenye sufuria yenye maji safi. Baadaye andaa mahitaji mengine kama kitunguu, karoti na pilipili hoho.

Ukipika nyama, subiri presha iishe kisha fungua mfuniko wa sufuria yako kisha changanya ndizi, viazi, viungo vyote na mafuta. Funika  tena na pika kwa muda wa dakika 10.

Muda wa kupika ukiisha ondoa presha kisha weka tui na acha ichemke kwa muda wa dakika 5 jiko likiwa wazi.  Chakula kitakuwa tayari na kipeleke mezani ukafurahie wewe na uwapendao.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa