Dk Mpango: Ongezeni matumizi ya nishati safi

Na Daniel Samson
13 Mar 2023
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema itasaidia kuongeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Tanzania.
article
  • Atoa agizo hilo kwa wakuu wa wilaya Tanzania. 
  • Nishati hiyo itasaidia kuokoa mazingira.

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema wakuu wa wilaya wanatakiwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika maeneo yao ili kuongeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Tanzania. 

Dk Mpango aliyekuwa akifungua mafunzo maalum kwa wakuu wa wilaya leo Machi 13, 2023 jijini Dodoma amesema dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayoanuai pamoja na uchafuzi wa mazingira. 

“Kasimamieni matumizi ya vyanzo vya maji na matumizi ya vyanzo mbadala ili kupunguza utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia,” amesema Dk Mpango.  

Vyanzo mbadala ni pamoja na matumizi ya nishati ya umemejua, bayogesi, gesi ya majumbani (LPG), jotoardhi na upepo ambavyo haviharibu mazingira. 

“Ili kuwa maendeleo endelevu Waheshimiwa wakuu wa wilaya zingatieni na kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na usafi katika maeneo yenu. Toeni hamasa kwa wananchi na hasa vijana ili wawe mstari wa mbele katika kushughulikia uhifadhi ikiwemo kupanda miti,” amesema.  

Hivi karibu Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia jijini Dar es Salaam alisema Tanzania imejiwekea malengo ya kufikia kiwango cha asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi na salama ifikapo 2032. 

Dk Mpango amesema ili kufikia lengo hilo, wakuu wa wilaya wanatakiwa kufanya kazi kwa karibu na taasisi za umma na sekta binafsi za nishati ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa