Sufuria zinazofaa kupikia katika jiko la gesi, umeme

Na Rodgers George
22 Oct 2021
Ni sufuria za chuma cha pua ambazo zinasifika kwa kudumu kwa muda mrefu hata zikitumika kwenye gesi.
article

  • Ni sufuria za chuma cha pua.
  • Ni rahisi kupikia na pia zinadumu kwa mudamrefu.
  • Kasoro yake ni vyakula kushika na kubadilika rangi zikitumika kwenye moto mkali kwa muda mrefu.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa mapishi katika jiko la gesi ni rahisi na salama kwa afya ya mpishi, yapo mambo mbalimbali ambayo yanaweza kumfanya mpishi akafurahia zaidi anachokifanya jikoni huku akibana matumizi ya nishati hapo hapo.

Ni pamoja na maujanja ya jikoni na vyombo ambavyo anavitumia ambavyo vitarahisisha utumiaji wako wa gesi au umeme wakati wa kupika.

Furaha yako inaanza na sufuria unazopikia

Kwa wengi, sufuria na mifuniko ya aluminiamu ndiyo habari ya mjini kwa mapishi yao kwani zinapatikana kwa bei rahisi na baadhi wanasema zinadumu kwa muda mrefu lakini leo nakuja na habari tofauti kidogo.

Sufuria na mifukiko ya aluminiamu ni miepesi zaidi, jambo linazifanya kuwa na “mushkeri” kwa matumizi ya familia kwani zinabondeka kwa haraka kulingana na utunzaji. 

Kwa familia, sufuria huoshwa walau kila siku na uoshwaji ambao unahusisha mgandamizo fulani. Bado hazijadondoka, hazijapigwa pigwa na watoto na hazijakandamizwa na vitu vizito.

Hilo linasababisha mifuniko kutofunika vizuri na hivyo kutoa nafasi ya mvuke kutoroka wakati wa kupika na hivyo chakula kutumia muda mrefu kuiva.

Sufuria zipi ni bora?

Katika mapishi ya nishati safi, unahitaji sufuria na vyombo vya kupikia ambavyo vinahifadhi joto kwa asilimia 100. Ambavyo mifuniko yake inaendana sawa sawa.

Sufuria za chuma cha pua zinasifika kwa kukaa muda mrefu bila kukunjika. Picha| Ubuy

Sufuria za chuma cha pua (stainless steel)

Tovuti inayoandika masuala ya ya vyombo vya kupikia, www.allcookwarefind.com imeandika sufuria za chuma cha pua hudumu kwa muda mrefu na ni ngumu pia.

“Sufuria la chuma litadumu kwa muda mrefu na hata kufikia kizazi kinachofuata,” imeandika tovuti hiyo.

Sufuria ya chuma pia zinachemka haraka na hivyo kutumia muda mfupi kupika chakula. Sifa nyingine ni urahisi wa kusafishika na haziharibiwi na chakula hasa vyakula vyenye hali ya asidi.

Licha ya ubora wake, waswahili walisema kizuri hakikosi kasoro. Kasoro ya sufuria hizi ni kuharibika rangi pale zinapotumika kwenye moto mkali, na chakula kugandiana wakati wa kupika na hivyo “kuzingua” katika baadhi ya mapishi ikiwemo samaki na mayai.

Hata hivyo, kasoro hizo haziondoshi uzuri.

Fuatilia makala yangu ijayo kujua mbinu za kurudisha mng’ao wa sufuria za chuma cha pua.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa