Mapishi rahisi ya mkate wa skonzi za kuku

Na Lucy Samson
11 Dec 2023
Badala ya kuuza skonzi za kawaida kwa Sh200 mpaka Sh500 unaweza kuongeza nyama ya kuku ukauza kwa Sh1,000 mpaka Sh2,000 kutegemea na eneo unalouzia vitafunwa vyako.
article
  • Aina hii ya mapishi inaweza kuongeza thamani ya biashara yako na kukuongezea kipato.
  • Ni pishi rahisi na huchukua muda mfupi kuiva.

Furaha ya kila mpishi ni uwezo wake wa kuongeza ubunifu katika pishi analoliandaa ili kuwafurahisha walaji.

Tunapomaliza mwaka 2023, JikoPoint tumekuandalia aina mpya ya upishi wa mkate maarufu wa skonzi, ambazo hupikwa pamoja na nyama ya kuku.

Kwa wauza vitafunwa migawahani au hotelini huu ndio wakati wa kujiongezea wateja na kipato kwa kuongeza aina mpya ya kitafunwa chenye ladha ya kipekee.

Badala ya kuuza skonzi za kawaida kwa Sh200 mpaka Sh500 unaweza kuongeza nyama ya kuku ukauza kwa Sh1,000 mpaka Sh2,000 kutegemea na eneo unalouzia vitafunwa vyako.

Karibu jikoni, tupike pamoja, nikuhakikishie kuwa kitafunwa hiki hakichukui muda mwingi jikoni, hivyo unaweza kupika kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani.

Hatua kwa hatua mapishi ya skonzi

Anza kuandaa unga wa ngano utakaotumika kuandaa skonzi. Hakikisha umenunua unga wa maandazi ili uweze kuumuka vizuri.

Chekecha unga kuondoa uchafu wote unaoweza kuwepo, kisha ongeza chumvi kiasi kulinganana wingi wa unga utakaotumia, weka hamira kiasi maji au maziwa ikiwa utapendelea. 

Kanda unga taratibu huku ukiongeza maji au maziwa kidogo kidogo mpaka uwe laini. Malizia kwa kuweka kiasi kidogo cha mafuta au siagi kisha acha uumuke kwa dakika 30 au zaidi.

Wakati unasubiri unga uumuke andaa nyama ya kuku iliyochemshwa kwa viungo (tumia nyama ya kuku kuendana wingi wa unga au mahitaji yako).

Changanya vipande vya kuku vilivyoiva na kutolewa mifupa, kitunguu na karoti kisha usage kwa kutumia blenda mpaka iwe laini. Ikiwa hauna blenda katakata nyama na viungo kwa saizi ndogo ndogo.

Baada ya hatua hiyo angalia kama unga umeshaumuka vya kutosha kwa ajili ya kuweka nyama ya kuku.

Tandaza ngano yako mezani au kwenye kibao, weka nyama ya kuku iliyosagwa kisha ugawe ngano kwa saizi ndogo ndogo na utengeneze umbo la duara.

Rudia hatua hiyo kwa ngano na nyama ya kuku iliyobaki, paka mafuta kwenye chombo cha kuokea na upange ngano yako uliyoitengeneza kwa maumbo ya duara.

Baada ya hapo choma kwenye oven au jiko la mkaa kwa dakika 30 mpaka 45 na skonzi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa