Chai ni kinywaji kinachotumiwa na wengi hususani wakati wa kifungua kinywa huku wengine wakikitumia kama kiburudisho wakati wa jioni na mchana katika maeneo yenye baridi.
Licha ya umaarufu wake maandalizi ya kinywaji hiki hutofautiana kati ya mapishi na mpishi au nchi na nchi.
Wapo wanaochemsha na majani ya chai yaliyokwisha kutengenezwa yanayopatikana katika maduka makubwa hata Yale madogo yanayopatikana mtaani.
Wapo walioenda mbali zaidi na kuongeza viungo mbalimbali na kufanya kinywaji hicho kivutie zaidi huku kikiimarisha afya zao.
Matumizi ya chai pia yanaweza kukupunguzia uchovu, wasiwasi, kuongeza umakini wa kazi na kuboresha utendaji kazi wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Mbali na faida hizo, tovuti ya Jamii Forum inasema kuwa matumizi ya majani ya chai ya kiwandani kuna athari zitokanazo na majani ya chai ambayo yanaweza kusababisha kansa,upotevu wa madini na vitamin mwilini, uchovu sugu na kisukari kutokana na kemikali ya ‘caffeine’ iliyopo katika majani hayo.
Ili kuepuka madhara hayo, leo tutajifunza jinsi ya kuandaa viungo vya chai bila ya kutumia majani ya chai ambayo unaweza ukayatumia kwa miezi miwili kwa gharama nafuu, huku ukiweza kunogesha chai yako kwa kuweka tangawizi, maziwa au mchaichai.
Tuingie jikoni
Hatua ya kwanza utaangalia viungo vyako kama vina mabaki ya uchafu ili viwe visafi, kisha utavichanganya kwa pamoja.
Baada ya kuhakikisha una viungo vyako vyote,saga mchanganyiko wako kwa kutumia blenda kwa muda wa dakika tano, ukimpumzika kila baada ya dakika moja ili kuepusha blenda kupata moto sana na kuharibika.
Itapendeza zaidi ikiwa utasaga kwa kutumia blenda inayotumia kusagia vitu vikavu.
Kama hauna blenda unaweza tumia kitwangio chako, utachukua viungo vyako na kuvikaanga kisha utavitwanga kwa pamoja ili kuweza kupata unga huo wa chai.
Utaendelea kusaga hadi viungo viwe laini kabisa, kisha utauhifadhi katika chombo kikavu kwa ajili ya matumizi ya kupikia.
Kama unatwanga kwa kinu uhakikisha unachekecha ili kuondoa mabaki ya viungo ambayo hayakutwangika vizuri.
Ili kuhifadhi vyema viungo hivi utalazimika kutumia chombo ambacho hakipitishi hewa ili usipoteze harufu na uhalisia wake ukiwa unatumia.