Mikunde ni miongoni mwa makundi ya chakula ambayo hujumuisha mazao ya chakula kama maharage,choroko, mbaazi, kunde na njegere.
Je unazifahamu faida za kiafya za kula mazao ya mikunde?
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) linaeleza kuwa ulaji wa aina hii ya chakula unaweza kuimarisha afya ya binadamu, mifugo pamoja na udongo kutokana na wingi wa virutubisho vilivyopo..
“Kwa wastani, kunde huwa na asilimia 19 hadi 25 ya protini, huku nyinginze zikizidi asilimia 30 ya protini…zao hili ni muhimu kwa watu ambao lishe zao hazihusishi ulaji wa nyama,” imesema taarifa ya FAO iliyochapishwa Februari 10, 2024.
Mbali na faida hizo,FAO inaeleza mikunde huweza kumuepusha mlaji na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na magonjwa ya moyo kutokana na zao hilo kuwa na kiwango kidogo cha mafuta na chumvi.
Mazao hayo pia husaidia kutunza mazingira kutokana na uwezo wake wa kuzalisha hewa ya nitrojeni ambayo inarutubisha ardhi, pia aina nyingi za mikunde huvumilia ukame, hivyo kuzalisha chakula hususan katika jamii zinazopata mvua chache.
Kwa upande wa Tanzania, ripoti ya hali ya chakula kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 inayotolewa na Wizara Ya Kilimo inabainisha kuwa mwaka 2021/2022, tani 2.1 za mikunde zilizalishwa sawa na asilimia 11.6 ya chakula chote kilichozalishwa nchini.
Kutokana na takwimu hizo,Tanzania ina ziada ya tani 1.2 ya zao la mikunde itakayotosha kwa matumizi na kuwahakikishia watanzania faida lukuki ikiwemo virutubisho vinavyoimarisha mwili.
Hata hivyo, FAO inasema pamoja na faida zote hizo, mikunde imepoteza umaarufu wake katika miaka ya karibuni na matumizi yake duniani kote yamepungua kwa sababu ya ongezeko la kipato miongoni mwa walaji na pia walaji kupendelea vyakula vingine zaidi ya mikunde.