Hawa ndio kuku wa ‘air fryer’

Na Lucy Samson
18 Apr 2023
Kuku huyu haihitaji mafuta mengi kwa sababu unakaangwa kwa joto la kifaa hicho.
article
  • Ni jiko la nishati safi linalotumia umeme.
  • Linarahisha mapishi ya nyumbani, mgahawani na hotelini.
  • Matumizi yake ni rahisi.

‘Air fryer’ ni moja kati ya vifaa vya kisasa vya mapishi vinavyotumia nishati safi ya kupikia.

Uwepo wake jikoni ni msaada mkubwa kwa wapishi majumbani, migahawani na hotelini ambapo huwapunguzia  muda wa kuandaa mapishi mbalimbali.

Ikiwa ni mara yako ya kwanza kukisikia kifaa hiki kinachosifika kwa kupika msosi kwa haraka,  usijali! JikoPoint tupo kwa ajili yako.

Jiko hili hutumia umeme kurahisisha shughuli mbalimbali za mapishi kama kuchoma, kuoka, kupasha hadi kukaanga kwa kutumia mafuta kidogo.

Kifaa hicho cha kisasa hutumia joto la juu na chini llitokanalo na umeme kuivisha chakula ambacho huwekwa kwenye sehemu ya chini ya bakuli la chuma linalopitisha moto.

Maandalizi

Hatu ya kwanza kabisa ni kuandaa kuku utakayemchoma kwa kukata kata na kumchanganya na  viungo unavyovipendelea (marinate)  na kumuacha kwa dakika 15 hadi 20 ili viungo viweze kuenea.

Baada ya muda huo kupita safisha ‘air fryer’ yako, kausha maji maji yanayoweza kuwepo tayari kwa kuanza kuchoma.

Nyunyizia mafuta kiasi kwenye bakuli la ‘air fryer’ ili kuku asishikane kisha weka vipande vya kuku vilivyokatwa katwa.

Ukimaliza  nyunyiza tena mafuta kwa juu na uweke moto wa kuchomea kiwango cha 140 mpaka 160 kwa dakika 15.

Ukishakadiria muda funga jiko na uruhusu lianze kuchoma kuku wako.

Baada ya dakika 15 fungua na ugeuze kuku wako,  kisha acha upande wa pili uive kwa dakika 15 nyingine.

Baada ya hapo, kuku wako atakawa amepata rangi ya kahawia (golden brown) ikiashiria ameshaiva na yuko tayari kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa