Jinsi ya kuandaa nyama ya ‘foil’

Na Lucy Samson
5 Dec 2023
Licha ya msosi huo kuuzwa sehemu mbalimbali, bado unaweza kujifunza kuundaa nyumbani ikiwa utafuatana nami hadi mwisho wa makala hii.
article
  • Sio lazima uwe na  vifaa vya kisasa kama ‘oven’ au ‘air fryer’ kuiandaa.
  • Unaweza kutumia nyama yoyote utakayopendelea.

Nyama ya ‘foil’ miongoni mwa aina maarufu ya mapishi ya nyama inayopendwa na watu wengi.

Utamu wa aina hii ya nyama huwafanya watu kutoboa mifuko hao kuanzia Sh4,500 hadi 10,000 ili kuipata katika hoteli, mikahawa na sehemu mbalimbali wanazouza chakula.

Kwa wasiofahamu nyama ya ‘foil’ ni aina ya upishi wa nyama unaohusisha ‘foil’ ambayo ni karatasi maalumu kwa ajili ya kufungia chakula pamoja na na kutunza joto.

Licha ya msosi huo kuuzwa sehemu mbalimbali, bado una nafasi ya kujifunza kuundaa ukiwa nyumbani kwako kwa muda mchache tu ikiwa utafuatana nami hadi mwisho wa makala hii.

Tuingie Jikoni

Hatua ya kwanza ni kuanda mchanganyiko wa viungo ambao unakuwa na tangawizi, kitunguu swaumu,kitunguu maji cha unga, chumvi, ‘vinegar’ au limao pamoja  na mafuta ya kupikia.

Kumbuka ili ‘foil’ yako inoge ni vyema kuweka nyanya, hoho, karoti na aina nyingine yoyote ile ya viungo unayopendelea bila kusahau papai ambalo hufanya nyama ilainike kwa haraka.

Baada ya hapo andaa kitoweo utakachotumia kwa kukiosha vizuri, chuja maji kisha uongeza papai ambalo hufanya kazi zaidi  likisagwa kwa kutumia blenda au kisagio cha mkono.

Mimina mchanganyiko wa viungo ulivyoandaa katika bakuli ya nyama kisha changanya vizuri ili vikolee.

Unaweza kuamua kuchanganya na viazi au nyanya chungu katika foil na mboga yakoikawa tamu zaidi.Picha|Savory Nothing.

Hatua inayofuata ni kuanza kuchoma nyama, unaweza kuchagua kuchoma kwa kutumia vifaa vya kisasa kama ‘oven’, ‘air fryer’, jiko la umeme  au jiko la mkaa la kuchomea nyama.

Choma kwa daika 30 hadi 45 ili ziive vizuri, kisha kata kata vipande na uanze maandalizi ya kuzichoma kwa mara ya pili kwa kutumia foil.

Kwenye bakuli safi utamimina nyama ulizokatakata, mchanganyiko wa viungo kama ulivyofanya mara ya kwanza, ‘soya sauce’ (kiungo cha mchuzi), karoti, hoho vitunguu au aina yoyote ya mboga mboga unayopendelea.

Changanya vizuri mpaka nyama ichanganyike na viungo, mimina nyama kwenye foil, funga vizuri kisha choma kwenye foil kwa muda wa dakika 40 mpaka saa1.

Ukifika hapo mboga yako itakuwa  tayari kwa kula, unaweza ukala kwa ugali, ndizi ua aina yoyote ya chakula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa