Jinsi ya kuandaa ‘omelett’, toasted bread na chai ya maziwa

Na Lucy Samson
4 Aug 2023
Katika makala hii utajifunza kuandaa  mayai ya kukaanga (omelett), mkate wa kuoka ( roasted bread), nyanya za kukaanga pamoja na chai ya viungo.
article
  • Kifungua kinywa rahisi kinachoweza kunogesha upendo hasa kwa wanandoa.
  • Unaweza ukawaandalia ndugu, jamaa na marafiki.

Chakula ni miongoni mwa sehemu ambayo mtu anaweza kuitumia kuonesha upendo na kuwaunganisha ndugu jamaa na marafiki.

Kwa mfano, huwa unajisikiaje pale mtu wako wa karibu awe ni mume,mke, mpenzi, rafiki au ndugu anapokuandalia chakula kitamu hususani wakati wa asubuhi?

Najua mpaka sasa jibu unalo, Francis Rwebogora  ambaye ni baba na mme, mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam ameiambia Jikopoint namna ambavyo amekuwa akitumia kifungua kinywa kunogesha upendo kwenye ndoa yake.

“ Na wababa niwaambie siri, amka siku moja asubuhi mapema muandalie mkeo chakula cha asubuhi utanishukuru baadae mwenzangu,” ameongeza francis.

Sio mbaya chakula cha asubuhi unachomuandalia umpendae kikawa cha tofauti kidogo, katika makala hii utajifunza kuandaa  mayai ya kukaanga (omelett), mkate wa kuoka ( roasted bread), nyanya za kukaanga pamoja na chai ya viungo.

Maandalizi

Hatua ya kwanza katika mapishi ya leo ni kuchemsha maziwa yatakayokuwa sehemu ya kifungua kinywa.

Washa jiko bandika kiasi cha maziwa uoendacho, ongeza viungo vya chai kama tangawizi, mdalasini hiriki na vingine kadri unavyopendelea kisha funika acha ichemke.

Wakati chai inachemka andaa mahitaji mengine yatakayotumika ikiwemo nyanya, kitunguu pamoja na karoti kama unapendelea.

Baada ya kuosha na kukakata, andaa mayai kwa kuyapasua kwenye bakuli safi, ongeza chumvi kiasi na uyakoroge hadi ya changanyike vizuri.

Anza kukaanga mayai kwa kubandika sufuria au kikaango jikoni kisha mimina mafuta ya kupikia kiasi na yakichemka weka vitunguuu maji na karoti kisha ukoroge mpaka vibadilike rangi.

Baada ya hapo mimina mayai na uache yaive kwa dakika 2 au zaidi kulingana na kiwango cha moto kisha geuza upande wa pili uive pia.

‘Omelett’ ikiiva epua na utumie sufuria hiyo hiyo kukaanga nyanya ulizoziosha na kukata saizi kubwa kwa dakika mbili mpaka tatu hadi zitakapoonyesha dalili ya kuiva weka chumvi na binzari nyembamba kisha uziepue.

Kumbuka awali tulibandika maziwa, hivyo huu ndio wakati wa kuyaangalia kama yamechemka yachuje na uweke katika chupa au vikombe tayari kwa kunywa.

Unaweza kuongeza sukari au ukatumia asali ikiwa haupendi sukari.

Kifungua kinywa cha leo kinakamilishwa na mkate ambao unaweza pia kuuoka ili kuonyesha utofauti wa kifungua kinywa chako.

Katika hatua hiii unaweza kutumia ‘bread toaster’ au ukatumia kikaango kwa kuuchoma upande upande hadi upate rangi ya kahawia kidogo ndipo utoe na utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mpaka hapo utakuwa umekamilisha maandalizi ya mapishi aina nne yani ‘Omelett’, chai ya maziwa, mkate wa kuoka (toasted bread) na nyanya za kukaanga ( fried tomatoes).

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa