‘Pressure cooker’ ni moja ya kifaa kinachotumika kwa ajili ya mapishi ya aina mbalimbali majumbani, migahawani pamoja na hotelini.
Wengine hupenda kuiita sufuria ya umeme, sifa kubwa ni uwezo wake wa kuivisha chakula kwa muda mfupi zaidi tofauti na kutumia sufuria za kawaida.
Mathalani, kama mtu hutumia saa moja kuivisha maharage kwa kutumia jiko na sufuria ya kawaida, basi kwa kutumia pressure cooker unaweza kutumia nusu ya huo muda au chini ya hapo.
Kifaa hicho cha mapishi kinachozidi kupata umaarufu kwa siku za hivi karibuni kinaweza kupika aina mbalimbali za vyakula ikiwemo vya vya nafaka kama maharage, aina mbalimbali za nyama na mboga za majani.
Ina faida kiafya.
Mgandamizo wa hewa (pressure) unaozalishwa na kifaa hicho huwezesha vyakula kuiva kwa haraka bila kupoteza virutubisho vya chakula husika kulinganisha aina nyingine ya kifaa cha umeme.
“Mvuke uliogandamizwa husaidia kutunza virutubisho vyote, utafurahia chakula chenye virutubisho na afya,” inasema tovuti ya kampuni ya Dessin ambayo huuza vifaa hivyo.
Baada ya kufahamu faida za kiafya za kutumia ‘pressure cooker’, fuatana nami ujifunze namna rahisi ya kutumia kifaa hicho kupika mchemsho wa nyama ya ng’ombe na viazi mviringo.
Maandalizi
Hakikisha ‘pressure cooker’ yako ni safi, imekaushwa maji tayari kwa kuanza mapishi. Andaa nyama, viazi, hoho, karoti, kitunguu kisha uoshee na ukate kwa saizi upendayo.
Baada ya maandalizi hayo chomeka waya wa pressure cooker kwenye umeme, wakati inawaka anza kwa kuweka nyama, tangawizi na kitunguu swaumu katika sufuria ya pressure cooker kisha mimina maji ya kulingana na wingi wa nyama na ufunike ili hewa isiingie
Kama viazi vyako ni vingi kuliko nyama au ni vigumu kuiva unaweza kuweka kuviweka wakati huu viive pamoja na nyama na kama sio vingi basi unaweza kuviweka wakati wa kuunga.
Hatua inayofuata ni kuweka muda, pressure cooker aina nyingi huwa na sehemu maalum inayoonesha aina ya chakula pamoja na muda utakaotumika kuivisha chakula hicho.
Mathalani mapishi ya nyama ambayo tutaandaa leo huhitaji dakika 25 mpaka dakika 45 kulingana na wingi wake.
Baada ya kuweka muda bonyeza kitufe kitakachoruhusu kuanza kwa mapishi yako. Subiri baada ya mpaka muda uishe ili uweke viiungo.
Ukihakikisha nyama na viazi vimeiva ongeza hoho,nyanya ya pakti au ya kusaga kama unapendelea, karoti, kitunguu, chumvi na viungo vya mchuzi kisha subiri kwa dakika nyingine mbili.
Baada ya hapo mchemsho wako utakuwa tayari kwa kuliwa.
Jipange
Pamoja na kuivisha chakula kwa haraka lazima utahitaji nishati ya umeme, hivyo walioko katika maeneo yasiyo na huduma hiyo wanaweza kupata changamoto.
Blogu ya ‘let’s save electricity’ inayojihusisha na kupima matumizi ya umeme inasema kila ‘pressure cooker huwa na kiwango tofauti na matumizi ya umeme kutokana na ukubwa na jinsi iliyotengenezwa.
“Pressure cooker nyingi zenye Wati kuanzia 700 mpaka 1,200 hutumia hadi uniti 18 kwa mwezi kama ikitumiwa kila siku kwa muda wa dakika 30,” imesema Blogu hiyo.