Pilau la prawns ni moja ya chakula ghali kama ambavyo vyakula vingine vinavyohusisha samaki vinavyouzwa katika baadhi ya hoteli na migahawa iliyopo nchini Tanzania.
Utamu na upekee wa chakula hiki ndio umewafanya walaji wake kutoboa mifuko yao zaidi ili kukinunua na kufaidi ladha yake iwe ni kwa ajili yao binafsi au familia.
Usichokijua ni kwamba unaweza kuokoa gharama hizo kwa kuamua kupika msosi huo nyumbani kwako kwa urahisi tu ikiwa utafuatana nami katika makala hii mwanzo hadi mwisho.
Tuandae prawns (kamba)
Mapishi ya pilau la prawns huanza kwa kuandaa prawns utakayemtumia kama kitoweo.
Ikiwa ni mara ya kwanza kupika prawns hakikisha unaondoa gamba gumu lililo nje ya samaki hao na uwaoshe kwa maji safi kwa ajili ya kuweka viungo ambavyo ni kitunguu saumu, tangawizi, chumvi, manjano, ndimu pamoja na binzari nyembamba kiasi.
Changanya viungo vyote na prawns ongeza mafuta au siagi kidogo kisha uache viungo vikolee kwa muda wa dakika 30 au zaidi.
Tuhamie kwenye pilau
Wakati viungo vinendelea kukolea kwenye prawns ndio wakati sahihi wa kuendelea na maandalizi ya pilau.
Hakikisha kabla ya kuwasha jiko umeandaa mchele, kitunguu maji, kitunguu saumu, karoti, hoho, tangawizi, chumvi, mafuta ya kupikia pamoja na viungo vya pilau.
Baada ya kuandaa na kusafisha viungo vyote vinavyohitaji kusafishwa washa jiko bandika sufuria jikoni kulingana na wingi wa chakula chako utakachopika.
Sufuria ikipata moto weka mafuta jikoni na yatakapochemka miminia vitunguu maji, kitunguu saumu na tangawizi iliyotangwa kisha ukoroge hadi vitakapobadilika rangi.
Hatua inayofuata baada ya hapo ni kuweka viungo vya pilau unavyopendeleakisha ukoroge vizuri vichanganyike na mafuta.
Kama unapenda kuweka viazi na njegere mbichi katika pilau huu ndio wakati wakati sahihi wa kuweka.
Dakika mbili au tatu baada ya kuweka viungo hivyo, weka mchele, chumvi na maji ya moto kiasi, koroga na uache uchemke kwa moto mdogo mdogo hadi ukaribie kuiva.
Weka prawns kwenye pilau
Ukihisi wali wako umeanza kuiva geuza na mimina prawns uliowaandaa awali kisha funika tena ili waive.
Ikiwa unatumia jiko la gesi au umeme huna haja ya kupalia na makaa, unachotakiwa kufanya ni kupunguza moto na kuacha uive kwa mvuke taratibu.
Chakula chako kikiwa kinaendelea kiva unaweza kuongeza hoho na karoti na mafuta kiasi ili kuleta ladha katika pilau. Wakati unaongeza viungo hivyo hakikisha kwanza kama prawns wako wameiva.
Dakika tano baadae chakula chako kitakuwa tayari, unaweza kuongeza kachumbari na juisi ili kukamilisha mlo wako.