Katika anga za mapishi kwa sasa, samaki ni chakula kisichoepukika jikoni. Pia samaki wa kupaka ni moja kati ya pishi pendwa kwa jamii zinazozungukwa na bahari, mito au maziwa.
Kutokana na muingiliano wa watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii pishi hilo unaweza kulipata kwenye hoteli yoyote lakini itakubidi kutoboa mfuko wako kupata msosi huo.
Kwa baadhi ya migahawa na hoteli za hali ya kati, msosi huo utaupata kuanzia Sh9,000 mpaka Sh14,000.
Unawezaje kumpika kiumbe huyu wa majini nyumbani? Fuatana nami katika hatua zote zote:
Maandalizi
Osha samaki vizuri na kuparua magamba (kama yakiwepo) kisha umuandae kwa ajili ya kupika pishi hili la samaki wa kupaka.
Ili kupata matokeo mazuri katika upishi huu wa samaki wa kupaka ni vyema kuanza kwa kumpaka viungo na kumloweka (marinate) kwa muda wa dakika 10 mpaka 20 kabla ya kuanza kumuunga.
Kwenye kibakuli kidogo changanya manjano kijiko kimoja cha chakula, pilipili ya unga kijiko kimoja, tangawizi nusu kijiko, kitunguu swaumu robo kijiko, chumvi robo kijiko, mafuta kijiko kikubwa kimoja na maji ya ndimu au limao kijiko kimoja.
Baada ya kuchanganya viungo vyote vizuri, mpake samaki ndani na nje kisha mfunike vizuri na umuache kwa dakika 10 au 20, pia unaweza kumuweka kwenye mfuko wa plastiki na kumuweka kwenye friji ili viungo viiingie vizuri.
Twende sasa jikoni
Wakati unasubiri viungo viingie kwenye samaki wako unaweza kuandaa mchuzi wa samaki.
Kwenye hatua hii utaanza kuandaa nyanya, kitunguu, karoti, tui la nazi kitunguu swaumu, tangawizi na hoho.
Washa jiko, bandika sufuria na uongeze mafuta kiasi tayari kwa kuandaa mchuzi utakaotumika kupaka samaki wako.
Mafuta yakichemka weka vitunguu maji, tangawizi, swaumu na ukoroge mpaka vipate rangi ya kahawia kisha ongeza nyanya na uache ziive.
Zikiiva ongeza karoti, hoho na tui la nazi na uache kwa dakika tano ichemke.
Wakati unasubiri ichemke anza kuchoma samaki wako kwa oven au kwa kupalia kwa moto wa mkaa ikiwa hauna oven.
Kwa njia yoyote ile utakayoitumia kumbuka kuanza na mafuta kidogo chini ya sufuria au kwenye wavu wa kuchomea samaki ili asishikane.
Samaki akiiva mtoe na umuweke pembeni kwa ajili ya kuanza kumpaka. Utahitaji sahani au bakuli kubwa ambalo samaki wako anaweza kutoosha.
Mchuzi ukishashemka anza kwa kupaka kwenye bakuli au sahani ikifuatia na samaki wako kisha umwagie mchuzi uliobakia kwa juu.
Mpaka hapo samaki wako atakuwa tayari kula kwa ugali, ndizi au chapati. Unasubiri nini? Sogea mezani na uwapendao.