Kwa nini ujifunze kupika kababu za nyama ya kuku?

Na Lucy Samson
28 Feb 2023
Pishi hili linaweza kutumika zaidi kwenye chakula cha familia na sherehe mbalimbali ikiwemo harusi.
article
  • Pishi linalowafaa zaidi wapenzi wa nyama nyeupe.
  • Linaweza kutumika zaidi kwenye chakula cha familia na sherehe mbalimbali ikiwemo harusi.

Nyama ya kuku ni moja kati ya kitoweo kinachosifika kwa kuwa na ladha tamu. Si ajabu kuona aina mbalimbali za mapishi yanayotokana na kitoweo hicho ikiwemo kababu.

Leo jikoni tunaandaa kababu ya nyama ya kuku. Pishi linalowafaa zaidi wapenzi wa nyama nyeupe.

Pishi hili linaweza kutumika zaidi kwenye chakula cha familia na sherehe mbalimbali ikiwemo harusi. Pia unaweza kujipikia pishi hili na kuwa sehemu ya mlo wako wa asubuhi, mchana au jioni.

Tusipoteze muda, tuingie jikoni 

Andaa nyama ya kuku kwa kuiosha na kuikata kata vipande vidogo vidogo. Hakikisha umetoa mifupa yote.

Baada ya hapo weka kwenye chombo kisafi kisha ongeza chumvi, viungo vya mchuzi (garam masala na paprika) pamoja na maji ya limao. Ongeza pia kitunguu swaumu na tangawizi kisha usage vyote pamoja kwenye blenda.

Ikiwa hauna blenda chemsha nyama ya kuku mpaka iive kisha ichambue upate vipande vidogo vidogo.

Baada ya hapo hatua inayofuata ni kutengeneza maumbo kwenye kababu zetu kwa ajili ya kuchoma.  Pia utahitaji mayai, chenga za mkate au tambi zilizovunjwa vunjwa kwa ajili ya kuweka nakshi.

Matumizi ya blenda kwenye upishi wa kababu hurahisisha maandalizi ya nyama kwa kuchemsha na kukatakata hivyo kuokoa muda.Picha | Tajiri’s Kitchen

Kwenye bakuli lenye nyama ya kuku iliyosagwa au kuchambuliwa vizuri ongeza mayai mawili au matatu kutokana na wingi wa nyama pamoja na majani ya dania kama unapendelea.

Koroga vizuri na utengeneze duara au umbo lolote unalopendelea, kisha upige mayai mengine matatu kwenye bakuli safi.  Ziimwagie chenga za mkate kisha uweke pembeni kwa ajili ya kuchoma.

Rudia hatua hiyo kwa kababu zilizosalia. Unaweza pia kuongeza vijiti vya mishikaki kwa chini ila hakikisha ni vifupi na vitaweza kuingia kwenye kikaangio chako.

Baada ya hapo choma kwa moto mdogo mpaka ziive vizuri. Baada ya hapo, msosi wako utakuwa tayari. Unaweza kusindikiza kababu zako kwa kinywaji ikiwemo juisi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa