Mapishi rahisi ya njugu mawe za sukari wakati wa Ramadhan

Na Lucy Samson
1 Apr 2023
Unaweza kuzitumia wakati wa kufuturu pamoja na chapati au maandazi.
article
  • Njugu mawe ni mboga nzuri unayoweza kuitumia wakati wa kufuturu.
  • Ni rahisi kuiandaa na haina mahitaji mengi.

Njugu mawe ni moja kati ya mboga jamii ya kunde zinazotumiwa na watu wengi hususani kufungulia kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan utasikia aina mbalimbali za mapishi ya njugu mawe yanayoweza kukushangaza.Kuna njugu mawe za mafuta, nazi, rosti, na sukari. Leo tunajikita katika upishi wa njugu mawe za sukari.

Maandalizi ya pishi hili hayatofauti sana na yale ya njugu mawe za kawaida zinazoungwa na nyanya. Pishi hili tunaongeza nazi na sukari na kulifanya linogeshe futari unayoiandaa.

Maandalizi

Chambua na kuondoa uchafu au mawe yanayoweza kuwepo kwenye nafaka hizo. 

Ukimaliza kuchambua zioshe na uweke kwenye sufuria safi na ubandike jikoni mpaka ziive.

Wakati unasubiri ziive andaa nazi. Unaweza kuikuna kwa kutumia kibao cha mbuzi, kuisaga kwa blenda au mashine nyingine za kisasa za kukuna nazi.

Zoezi la kukuna nazi likimalizika ichuje  na utenganishe matui mawili  zito na jepesi kulingana na wingi wa nazi yako. Unaweza pia kutumia nazi ya pakiti ambayo haiitaji maandalizi mengi.

Menya hiriki na uitwange pamoja na sukari kiasi utakayoitumia kwenye njugu mawe zako.

Baada ya njugu mawe kuiva anza kwa kuweka tui jepesi, iriki na sukari, koroga kisha uache mpaka tui lianze kukauka.

likikauka ongeza tui zito la pili, chumvi kiasi na mafuta kiasi kisha uchanganye vizuri na auache zichemke.

Zikishachemka kwa dakika tano mpaka 10 njugu mawe zako zipo tayari kuliwa. Unaweza kuzitumia wakati wa kufuturu pamoja na chapati au maandazi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa