Njia rahisi ya kupika pilau mayai

Na Mlelwa Kiwale
25 Jul 2024
Pilau ni miongoni mwa vyakula maarufu nchini Tanzania, umaarufu wa chakula hicho ulitokana na umaalumu wake, ambapo miaka ya nyuma ilikuwa kikiliwa haswa wakati wa sikukuu au wakati wa sherehe kama harusi. Pamoja na kwamba huenda mvuto wa chakula hicho ukawa umepungua kwa kiasi fulani kutokana na upatikanaji wake kuwa rahisi hivi sasa bado haibadili […]
article
  •  Ni chakula maarufu katika Mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi na mataifa ya Mashariki ya Kati na Asia.
  • Mayai hutumika kama mbadala wa  nyama au viazi.
  • Unaweza kuila nyumbani au kwa matumizi ya biashara.

Pilau ni miongoni mwa vyakula maarufu nchini Tanzania, umaarufu wa chakula hicho ulitokana na umaalumu wake, ambapo miaka ya nyuma ilikuwa kikiliwa haswa wakati wa sikukuu au wakati wa sherehe kama harusi.

Pamoja na kwamba huenda mvuto wa chakula hicho ukawa umepungua kwa kiasi fulani kutokana na upatikanaji wake kuwa rahisi hivi sasa bado haibadili uhalisia kuwa ni chakula pendwa hususan kwa watu wanaopenda vyakula vya kunukia na mchanganyiko wa viungo.

Pilau hupikwa kwa kuchanganya mchele, pamoja na viungo mbalimbali kama mdalasini, hiriki, binzari nyembamba, binzari manjano, karafuu, majani ya bay, pamoja na tangawizi ya unga ingawa wengine huongeza viungo vingine kutegemeana na matakwa ya mpishi na walaji wake.

Mlo huu ni maarufu hasa katika maeneo ya Mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi, Mashariki ya kati, Asia ya Kati, Asia ya Kusini, Afrika ya Mashariki, Latini Amerika na Karibian ambapo hupikwa kwa kujumuisha aina mbalimbali za nyama na mboga mboga ambavyo huleta ladha maradufu. 

Hata hivyo, leo tutajifunza aina nyingine ya upishi wa pilau kwa kutumia mayai ambayo hutumika kama mbadala wa nyama au viazi ambapo pilau lako likiiva unaweza kula na matunda, kachumbari, mboga za majani au pilipili.

Tuingie jikoni

Hatua ya kwanza ni kuchemsha mayai ambapo utachukua mayai yako matano au zaidi kwa kilo moja ya mchele, utayaweka katika sufuria yenye maji kiasi kisha nyunyizia na chumvi kwenye hayo maji ambayo unachemshia mayai yako kwa dakika 15.

Wakati ukisubiri mayai yako yaive, anza kuandaa mchele wako kwa kuuchambua vizuri na kuandaa viungo vya kupikia katika pilau lako. 

Utachukua vitunguu maji vitatu, nyanya moja ya kusaga au ya pakti, hoho moja, karoti moja, kitunguu saumu, tangawizi pamoja na binzari nyembamba(uzile) iliyosagwa pamoja, njegere kikombe kimoja kidogo, chumvi, binzari masala, curry powder, royco, maji ya uvuguvugu na viungo vya pilau (viungo hivi vinapatikana madukani kote au unaweza tengeneza mwenywe).

Hatua inayofuata ni kubandua mayai yaliyoiva na kuweka pembeni, baada ya hapo utachukua sufuria na kuweka mafuta kiasi kisha utaweka vitunguu vya maji ulivyovikata na utavikaanga hadi vibadilike na kuwa na  rangi ya kahawia.

Baada ya hapo utaweka mchanganyiko wa kitunguu saumu, tangawizi na binzari nyembamba ulizozisagia pamoja utakoroga na kuweka nyanya vijiko viwili au vitatu, chumvi, royco, binzari masala, curry powder, viungo vya pilau vyote utaweka vijiko viwili kwa kila kiungo.

Ongezea karoti na hoho kisha utachanganya vizuri na kuweka mchele, utakoroga na kumimina maji kiasi, changanya mchele na viungo kisha funika kwa muda wa dakika 15 ambapo utageuza na kuweka mayai uliyomenya na utafunika tena mpaka pilau yako itakapoiva.

Mpaka kufikia hapo pilau ya mayai itakuwa tayari kwa kuliwa ambapo unaweza kulia na kachumbari, matunda na pilipili ambapo unaweza kufurahia nyumbani na familia au kwa matumizi ya biashara.

Angalizo

Ni muhimu kuhakikisha moto ni wa wastani ili chakula kisiungue hususan kwa wale wanaotumia jiko la gesi au umeme na kwa wale wanaotumia jiko la mkaa wanazeza kupalilia ili chakula kiive vizuri.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa