Viazi maua: Pishi la kumpikia umpendae siku ya wapendanao

Na Fatuma Hussein
13 Feb 2024
Baada ya kuona faida za kumpikia umpendae sasa tusogee jikoni tujifunze namna rahisi ya kuandaa viazi maua vitaakavyonogesha zaidi upendo.
article
  • Mapishi ni miongoni mwa namna bora za kunogesha upendo aina ya wapendanao.
  • Aina hii ya mapishi inaweza kupunguza gharama za kula hotelini na migahawani katika siku ya wapendanao.

Umeshawaza msosi utakaomuandalia umpendae katika msimu huu wa sikukuu ya wapendanao?

Sahau kuhusu ratiba za kununua chakula mgawahani au kumpeleka katika hoteli ambazo zitafanya mifuko yako itoboke zaidi, zipo aina nyingi za misosi mitamu unayoweza kumuandalia ukiwa nyumbani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mpasho, kupika ni miongoni mwa namna ya kuonyesha upendo hususan kwa watu wenye mahusiano ya karibu.

“Wapo wanaosema njia pekee ya kuufikia moyo wa mwanaume ni kupitia chakula kizuri, nadhani kanuni hiyo inafanya kazi pande zote mwanamke pia anahitaji kupikiwa chakula kizuri, hii huongeza upendo na ukaribu zaidi,” inasema tovuti hiyo.

Baada ya kuona faida za kumpikia umpendae sasa tusogee jikoni tujifunze namna rahisi ya kuandaa viazi maua vitakavyonogesha zaidi upendo.

Jinsi ya kuandaa

Maandalizi ya viazi maua huanza kwa kumenya viazi mviringo (kiasi unachohitaji) kisha kata vipande vyembamba sana mfano wa ‘crips’ au kwa umbo la duara.

Unaweza kutumia kisu kikali au kifaa maalum cha ‘crips’ ambacho huuzwa kwa Sh1,000 au zaidi katika masoko mengi nchini.

Baada ya hapo viweke kwenye chombo kisafi, weka chumvi kiasi  na uviache kwenye maji kwa dakika 15 mpaka 20, lengo la kuweka chumvi ni kuvilainisha tayari kwa kuvikunja kutengeza maumbo ya maua,.

Muda huo ukiisha vitoe, na ukitaka kujua kuwa vipo tayari  ukivishika utaona vimekuwa laini na ukivikunja vinakunjika vizuri kabisa bila kukatika.

Tuendelee na maandalizi kwa kuvipitisha kwenye unga, unaweza kutumia aina yoyote ya unga iwe ngano, unga wa sembe au dona lengo ni kuvikausha baada ya kuvitoa kwenye maji.

This image has an empty alt attribute; its file name is jdoceocbfjbvfvofvbifbvibvbvroivboirbtrbrbgbgt-1024x784.jpg
Unaweza ukatengeza aina yoyote ya rosti utakayoisindikiza na pishi hili kwa kutumia nyanya, kitunguuu, karoti, kitunguu swaumu na viungo vyovyote unavyopendelea.Picha|FatumaHussein.

Ukimaliza hatua hiyo anza kuvikunja viazi vyako kwa mfano wa ua (waridi) kwa kutumia vijiti au ‘toothpick’, rudia hatua hiyo kwa viazi vyote ulivyoviandaa.

Hatua inayofuata ni kuandika kikaango jikoni, weka mafuta ya kutosha na yakichemka uanze kuvikangaa viazi maua ulivyovitengeneza kwa dakika mbili mpaka tatu hadi vitakapokuwa rangi ya kahawia.

Tumia moto mdogo mdogo ili usiharibu rangi nzuri ya kahawia ambayo ndiyo hufanya pishi hili kuwa na mvuto.

Baada ya hapo pishi lako litakuwa tayari, unaweza kuandaa nyama rosti au mboga yoyote ya pembeni kunogesha pishi  lako, bila kusahau kinywaji baridi.

Malizia kwa kuipamba vizuri sahani wakati unaandaa chakula mezani, unaweza kutumia majani ya mnanaa(mint) au giligilani.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa