Vyakula vya kula au kutokula wakati wa Ramadhani

Na Lucy Samson
23 Mar 2023
Wapo wanaofungulia kwa vyakula vyepesi kama chai, uji au maziwa lakini pia wapo wale wanaofungulia kwa vyakula vizito pasipo kujua madhara yake kiafya.
article
  • Ni pamoja na vyakula vyepesi na matunda. 
  • Epuka kula vyakula vya mafuta mengi.
  • Zinagatia ulaji wa ulaji wa mlo kamili

Kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani ni moja ya jambo ambalo linawawezesha Waislamu kujiweka karibu na kuimarisha imani yao na Mungu.

Kwa mujibu wa maandiko ya Quran tukufu, kufunga mwezi wa Ramadhani ni moja kati ya nguzo kuu tano za Uislamu ambazo kila muumini hutakiwa kuzitimiza katika maisha yake.

Katika kipindi hiki waumini hufunga kwa saa 12 kuanzia alfajiri mpaka magharibi ambapo hufungulia kwa aina mbalimbali za vyakula.

Wapo wanaofungulia kwa vyakula vyepesi kama chai, uji au maziwa lakini pia wapo wale wanaofungulia kwa vyakula vizito pasipo kujua madhara yake kiafya.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) vipo vyakula vinavyofaa na visivyofaa kuliwa wakati wa kufungulia katika msimu huu wa Ramadhan ikiwemo vyakula vyenye chumvi nyingi.

TFNC inasema vyakula vyenye chumvi nyingi vinaweza kukausha maji maji mwilini na kumsababishia mtu kiu zaidi ya maji na hivyo kushindwa kufunga siku inayofuata.

Vyakula vyepesi

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya na lishe, inashauriwa kula vyakula vyepesi wakati wa kufungulia na si vigumu, kwa sababu vyakula vigumu husababisha matatizo mbalimbali ya kiafya.

Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya Hamad ya nchini Qatar, ulaji wa vyakula vingi vigumu husababisha matatizo ya mfumo wa chakula, kisukari na unene uliopitiliza. 

Vyakula vyepesi unavyoweza kutumia wakati wa kufungulia ni pamoja na tambi, supu, mtori na vinywaji kama uji, chai au maziwa.

Ikiwa upo katika mazingira ambayo huwezi kupata chakula au vinywaji hivi unaweza kutumia maji kabla ya kula vyakula vingine

Chapati za kusukuma, chapati za maji, maandazi ni moja ya vitafunwa maarufu vinavyotumiwa kipindi cha mwezi wa Ramadhani. Picha | Rukia Lialatia.

Vyakula vya moto

Hata wakati ukila vyakula vyepesi, inashauriwa vyakula hivyo viwe vya moto ili kushtua tumbo (‘warm-up’) kwani linakuwa limekaa muda mrefu pasipo kupata chakula.

Matumizi ya nishati safi kama mashine ya kupashia chakula (‘microwave), jagi la kupashia maji la umeme (‘heater), majiko ya gesi na umeme yanaweza kukurahisishia kula chakula cha moto wakati wote wa wa Ramadhan.

Matunda 

Matunda yaliyokauka kama vile tende ni muhimu sana kipindi hiki cha Ramadhan kwani huupa nguvu mwili na kujaza tumbo kwa muda mrefu.

Kula tende wakati wa kufuturu (kufungulia) sio maadili ya kidini pekee, bali hushauriwa na wataalam wa afya ili kujenga afya bora.

Matunda mengine unayoweza kuyatumia msimu huu ni pamoja na ndizi, nanasi, papai, matikiti maji na matunda mengine kama hayo.

Chakula cha usiku (daku) hutakiwa kuwa mlo kamili wenye virutubisho vitakavyoupa mwili nguvu kwaajili ya funga ya siku inayofuata. Picha | Times Majira.

Zingatia haya

Zingatia kunywa maji ya kutosha wakati wa kufungulia ili kuwezesha mwili kuwa na maji ya ziada yakayokupa nguvu wakati wote ukiwa umefunga.

TFNC inasema  kushiba sana au kula kupita kiasi kunaweza kuzuia au kuzorotesha mchakato wa umengenywaji wa chakula tumboni.

Pia taasisi hiyo imetaka waumini wa kiislamu wanaofunga Ramadan  kupunguza kula vyakula vyenye mafuta mengi vinavyoweza kuongeza hamu ya kunywa maji na kukuzuia kufunga siku inayofuata.

Sambamba na hayo hakikisha futari (chakula kinachotumiwa wakati wa kufungulia) kinajumuisha makundi muhimu yaani protini, wanga, mafuta mbogamboga na matunda.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa