Zege Ndizi: aina mpya ya msosi inayovutia wengi

Na Mlelwa Kiwale
2 Aug 2024
Si watoto wala watu wazima wasiofahamu kuhusu chipsi zege hapa nchini kwetu. Urahisi wa kuandaa na ladha yake ndiyo kivutio kikuu kwa watu wengi kuchagua msosi huu pale wanapotembelea hotelini na sehemu nyingine zinazouzwa chakula. Vipi leo nikikutonya kuwa unaweza kuandaa zege kivingine kwa kutumia ndizi mbivu au mbichi? Usijiulize sana jikopoint leo imekuletea mapishi […]
article
  • Maandalizi yake hayatofautiani sana na chipsi zege
  • Unaweza kutumia aina yoyote ya ndizi unayopendelea

Si watoto wala watu wazima wasiofahamu kuhusu chipsi zege hapa nchini kwetu.

Urahisi wa kuandaa na ladha yake ndiyo kivutio kikuu kwa watu wengi kuchagua msosi huu pale wanapotembelea hotelini na sehemu nyingine zinazouzwa chakula.

Vipi leo nikikutonya kuwa unaweza kuandaa zege kivingine kwa kutumia ndizi mbivu au mbichi?

Usijiulize sana jikopoint leo imekuletea mapishi rahisi ya ndizi zege unazoweza kuandaa nyumbani au katika sehemu yako ya biashara.

Maandalizi 

Hatua ya kwanza ni kuchagua aina ya ndizi unaozitaka kutumia au zinazopatikana kwa urahisi katika eneo lako, iwe ni mzuzu,bukoba au malindi zote zinaweza kufaa katika aina hii ya mapishi.

Anza mapishi yako kwa kumenya ndizi na uzikate katika vipande vidogo vidogo itapendeza zaidi kama utakata umbo la duara kisha uvioshe na uendee kuandaa viungo vingine kama kitunguu, karoti na hoho.

Ukimaliza chuja maji kwenye ndizi hakikisha zimekauka kabla ya kuwasha jiko na kuzikaanga mpaka ziwe na rangi ya kahawia ndio utoe na kuchuja mafuta.

Rudia hatua hiyo mpaka ndizi zote ulizoziandaa ziishe kisha hamia kwenye kuandaa zege.

Hatua hii inafanana kabisa na Ile ya chipsi zege, cha kufanya ni kupasua mayai na kuyakoroga mpaka yachanganyike vizuri.

Ongeza viungo kaka hoho, karoti, vitunguu, chumvi na pilipili manga kama unapendelea kisha uendelee na hatua ya kukaanga ambapo utaanza kwa kuweka ndizi katika kikaangio (frying pan) kisha utamimina mayai na kuyasambaza yaenee katika kikaangio chote.

Baada ya kumimina utasubiri mpaka upande wa pili uive ndio utageuza  na baada ya dakika kama tatu au nne utageuza tena kuangalia kama pande zote zimeiva.

Wakati wote wa mapishi ya msosi huu hakikisha unapika kwa wastani ili ndizi pamoja na mayai yaive vizuri.

Ukiona ndizi zege imeanza kupata rangi ya kahawia hapo itakuwa tayari kwa kuliwa ikisindikizwa na kachumbari, mbogamboga na hata soda.

Kama ilivyo kwa chipsi zege, msosi huu pia unaweza kutumiwa muda wowote iwe asubuhi, mchana au jioni.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa