Gesi ya majumbani (LPG) ni miongoni mwa nishati safi na salama za kupikia ambazo zimekuwa zikichagizwa kutumiwa majumbani na katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Gesi hii huokoa muda na kumuepusha mtumiaji na madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa ikiwemo kansa na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) matumizi ya nishati za kupikia zisizo salama kama kuni yanaweza kusababisha matatizo mengine hatarishi kama matatizo ya uzazi kwa wanawake na magonjwa ya moyo.
Ripoti nyingine ya shirika hilo inaweka wazi kuwa takribani watu milioni 3.2 duniani kote walifariki mwaka 2020 kutokana na uchafuzi wa hewa majumbani unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa huku idadi ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano ikiwa 237,000.
Katika kupunguza athari zitokanazo na matumizi ya nishati za kupikia zisizo salama Wizara ya Nishati nchini Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Nishati Safi ya Kupikia ina mpango wa kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanahamia katika matumizi ya nishati safi ikwemo matumizi ya gesi kufikia mwaka 2030.
Baada ya kufahamu yote hayo tujifunze mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutumia nishati safi za kupikia hususani gesi
1. Tumia moto kiasi
Unapotumia gesi kupika au kuchemsha maji hakikisha unaruhusu gesi itoke kwa kiwango cha kawaida kutoka kwenye mtungi. Hii itasaidia kupata moto wa kawaida kuivisha chakula au kuchemsha maji kwa urahisi.
Ukiacha gesi itoke nyingi kwa wakati mmoja inaweza kuisha haraka na kukulazimu kutumia moto mkubwa bila sababu.
2. Tumia sufuria za kisasa
Siyo kila sufuria unaweza ukatumia katika jiko la gesi. Hivyo ni muhimu kuchagua sufuria inayofaa au chombo ambacho unaona ni imara kupikia.
Mara nyingi, sufuria ya kisasa ni ngumu na huwa si rahisi kuunguza chakula ukilinganisha na sufuria nyepesi zinaweza kusababisha chakula kuwahi kuungua.
3. Hakikisha unasafisha jiko lako kila inapobidi
Usafi wa jiko la gesi ni muhimu mara baada ya kupika. Unapaswa kuacha jiko lako likiwa limesafishwa na kuondoa uchafu ambao huenda ulidondoka wakati unapika.
Uchafu unaweza ukasababisha kuziba kwa matundu ya gesi hivyo kusababisha gesi kutotoka vizuri wakati unatumia jiko lako la gesi, hivyo hakikisha unasafisha jiko lako angalau mara moja kwa mwezi kama ilivyoshauriwa na tovuti ya Toshiba.
4. Chunguza kama kuna sehemu gesi inavuja
Mara kadhaa baadhi ya watu huhisi harufu ya gesi majumbani mwao. Hii inaweza kuwa ishara kuwa gesi inavuja mahali, inaweza kuwa mpira haujafungwa vizuri au sehemu ya jiko imeharibika na hivyo kuruhusu gesi itoke.
Kwa mujibu wa kampuni ya gesi ya kupikia Taifa Gas, endapo utahisi gesi inavuja hatua ya kwanza ni kufunga ‘regulator’ au sehemu ya kuwashia gesi kisha kufungua madirisha na milango ili hewa ipite.
Ikiwa unahisi bado gesi inavuja unaweza kutafuta fundi kwa ajili ya uchunguzi na matengenezo ili kukuepusha na madhara yanayoweza kutokea ikiwemo gesi kulipuka.
5. Usizidishe muda wa kutumia gesi yako
Huenda umebandika maji au chakula jikoni basi hakikisha upo karibu ili chakula kikiiva au maji yakichemka uweze kuyatoa jikoni.
Ukiacha moto kuwaka kwa muda mrefu bila kudhibiti kutachangia gesi kuisha mapema.
Endapo utazingatia mambo haya unapotumia jiko lako la gesi basi utakuwa miongoni mwa watumiaji bora na pia unaweza kuwashawishi watumiaji wengine kuzingatia kanuni hizi wakati wanatumia gesi.