FAO: Nyama ikiingia mezani, mikunde hunyanyapaliwa

Na Daniel Samson
23 Feb 2023
Mazao ya mikunde kama njegere, mbaazi, choroko, kunde yana umuhimu mkubwa kilishe, kiuchumi na kimazingira kwa sababu inarutubisha udongo.
article

Shirika hilo lasema mazao jamii ya mikunde hayapewi kipaumbele kwenye lishe nchini.


Jamii ya mikunde! Wengi wanaitambua zaidi kama ni kunde zenyewe, na maharagwe lakini ni zaidi ya hiyo. 

Kuna choroko, mbaazi, dengu na njegere ambapo kutokana na umuhimu wake siyo tu kiuchumi bali pia katika lishe ya binadamu, kurutubisha udongo na pia kuhimili mabadiliko ya tabianchi. 

Kutokana na umuhimu wake kwa mazingira na afya, Umoja wa Mataifa (UN) umekuwa ukihimiza matumizi ya nafaka hizo hasa katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za lishe. 

Nchini Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo (FAO) linafadhili mradi wa AgriConnect ambao unapawatia wananchi; wanawake na wanaume stadi za mapishi sahihi ya jamii ya mikunde.

“Vyakula vya jamii ya mikunde huondoka mezani pale nyama inapoonekana, vinanyanyapaliwa,” alinukuliwa Afisa lishe wa FAO nchini Tanzania Stella Kimambo hivi karibuni akiwa mkoani Njombe.

Kimambo akihojiwa na kituo cha mawasiliano cha UN, amesema idadi kubwa ya Watanzania hula zaidi maharage lakini mikunde kama vile mbaazi, dengu na choroko havipati nafasi mezani.

Ulaji uko chini lakini uuzaji mikunde nje ya nchi unazidi kupaa kila mwaka.

Umuhimu wa mazao hayo

Afisa Lishe kutoka Wizara ya Kilimo, Magreth Natai amesema mazao ya mikunde kama njegere, mbaazi, choroko, kunde ni mazao ambayo yana umuhimu mkubwa kilishe, kiuchumi na kimazingira kwa sababu inarutubisha udongo.

Amesema wataendelea kushirikisha wananchi kutambua umuhimu huo ikiwemo kwa lishe.

Ili kushamirisha ulaji wa mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini, FAO inaunga mkono mradi wa AgriConnect unaochagiza siyo tu kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao katika mikoa ya Nyanda za Juu za Kusini ikiwemo Njombe, bali pia kuhakikisha kuna uhakika wa chakula na lishe.

Watumia mashindano kuongeza hamasa

Mashindano ya upishi wa mazao ya mikunde yalifanyika mkoani Njombe Februari 10 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikunde Duniani. 

Mpishi na mama lishe wa mkoani Njombe Esther Lukasi  aliyeibuka mshindi wa pili katika mashindano hayo alipatiwa zawadi ya mtungi wa gesi, vijiko vikubwa vya chakula pamoja na kisu.

“Nilipika mchanganyiko wa wali na choroko, pilau la maharage, ugali wa maharage au usuge, mboga za majani na keki kwa kutumia ndizi na maharage,” amesema Lukasi akihojiwa na KidsTime FM ambyo ni redio mshirika wa UN.

Mashindano hayo yalikuwa kitu kikubwa kwake kwani hawajahi kupika vitu kama hivyo.

 “Ninashukuru FAO kwani wamekuja kutupa mafundisho ambayo hatukufahamu hapa. Na nina furaha sana sikutegemea kushinda na nimefurahi kuwa nitaweza kupika chakula kwa urahisi nyumbani kwangu,” amesema Lukasi. 

Licha ya Njombe kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi Tanzania, bado unakabiliwa na kiwango cha juu cha udumavu kwa watoto. 

“Tumeondokana na asili, zamani wazee wetu walipika kande, maboga lakini sisi tunaona uvivu kupika kwa muda mrefu. Hivyo ni vema turejee asili ili watoto wetu waweze kuwa na lishe bora,” amesema Sara Mtibike, mfanyabiashara katika soko la nafaka mkoani humo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa