Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia huku akibainisha kuwa lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati hiyo miaka 10 ijayo halitakuwa rahisi sana.
Serikali imeweka lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033 ili kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama ikiwemo kuni na mkaa zinazoathiri mazingira na afya za watumiaji.
Tanzania ni miongoni mwa nchi Afrika zenye kiwango kikubwa cha matumizi ya kuni na mkaa kupikia licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha nishati safi za kupikia kama gesi asilia, umeme, bayogesi na gesi ya kupikia (LPG).
Ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa kaya tisa kati ya 10 au asilimia 91 ya kaya zote Tanzania Bara hutumia kuni kama chanzo kikuu cha nishati kwa ajili ya kupikia.
Kutokana na takwimu hizo, Tanzania bado ina safari ndefu ya kuongeza matumizi ya nishati safi mara tisa zaidi ya kiwango cha sasa cha asilimia tisa iliyopo hadi asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka 10.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo (Mei 8, 2024) katika uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati ya Kupikia jijini Dar es Salaam amesema ili kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama nchini juhudi za pamoja zinahitajika ikiwemo kuelimisha wananchi juu ya faida ya nishati safi.
“Tatizo la matumizi madogo ya nishati safi ya kupikia ni mtambuka na ni suala linalohitaji nguvu za pamoja, hivyo mkakati huu unatoa mwongozo wa kitaifa kwa watu wote kufikia lengo tulilojiwekea la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa mkakati huo uliozinduliwa leo utanusuru maisha ya Watanzania na kuchochea jitihada za Serikali kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukataji miti ambapo hekta 469,000 zinakadiriwa kuteketea kila mwaka.
Awali, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, asema tayari baadhi ya taasisi zinazolisha watu 100 na kuendelea zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia huku akibainisha mipango ya kisera ya kuimarisha matumizi ya nishati hiyo.
“Tunaandaa, tunaoanisha na kuhuisha sera, sheria, kanuni na miongozo tuliyonayo iendelee kuwa wezeshi kwa wote ambao wanaoanza kutoa huduma za matumizi ya nishati safi na namna ya kupata nishati hiyo,” amesema Majaliwa.
Wadau wa sekta binafsi wakabiziwa zigo
Kutokana na ukubwa wa matatizo ya matumizi ya nishati zisizo salama, Rais Samia amewataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali ili kusambaza mitungi ya gesi na elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi za kupikia.
“Kila mdau ana nafasi ana jukumu katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati hu, kwa upande wa Serikali tunalo jukumu la kuongeza uelewa kwa wananchi,” amesema Rais Samia.
Miaka ya hivi karibuni Serikali na wadau mbalimbali wa nishati safi wameongeza jitihada za kuelimisha jamii ili kupunguza matumizi ya kuni, mkaa na nishati nyingine zisizo salama.
Miongoni mwa wadau hao ni Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, inayomiliki vyombo vya habari vya mtandaoni vya Nukta Habari na Jiko Point ambavyo huchapisha mara kwa mara maudhui yanayosaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka wadau hao kubuni namna rahisi na nafuu itakayowawezesha Watanzania hususani wa vijijini kuipata huduma hiyo kulingana na uwezo wa vipato walivyonavyo.