Utapiamlo hutafsiriwa kama hali mbaya ya kiafya ambayo hutokana na upungufu kupindukia au wa kadri wa virutubisho muhimu katika mwili wa mwanadamu.
Virutubisho hivyo ni pamoja na wanga, protini, mafuta, madini na vitamini ambavyo vikipungua husababisha ukondefu, uzito pungufu kwa watoto, kupungua kwa kinga ya mwili, macho kutoona vizuri, ugumba au upungufu wa damu.
Wakati mwingine utapiamlo unaweza kusababisha vifo hususani kwa wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto (THDS-MIS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano Tanzania wana udumavu.
Hiyo ni sawa na kusema katika kila watoto 10 nchini Tanzania watatu kati yao wana udumavu.
Ripoti hiyo imefafanua zaidi kuwa asilimia 3.3 ya watoto wana ukondefu na asilimia 12 wana uzito pungufu huku asilimia nne wakiwa na uzito uliopitiliza.
Hata hivyo, miongoni mwa sababu kubwa inayochochea uwepo wa utapiamlo ni kutokula chakula chenye virutubisho muhimu ambapo ripoti ya Global Hunger Index ya mwaka 2022 inaonesha asilimia 30.3 ya watoto walio chini ya miaka mitano katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara wana utapiamlo.
Madhara ya utapiamlo
Ripoti ya Lishe Duniani ya mwaka 2018 inaonesha kuwa, takribani watoto milioni 150.8 sawa na asilimia 22.2 ya Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano walikuwa wamedumaa na watoto milioni 50.5 sawa na asilimia 7.5 walikuwa na uzito pungufu.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kutokana na utapiamlo watu wazima milioni 462 walikuwa na uzito pungufu huku uwiano kati ya uzito na urefu (Body Mass Index) ukiwa chini ya 18.5.
Kwa ujumla, upungufu wa vitamini na madini unakadiriwa kuadhiri watu wapatao bilioni 2 duniani kote mwaka 2018, huku zaidi ya watu wazima bilioni 2 wakiwa na uzito uliozidi.
Idadi ya watu walioripotiwa kuwa na uzito uliozidi kutokana na utapiamlo ni sawa na moja ya tatu wa watu wazima wote ulimwenguni.
Kutokana na takwimu hizo ni wazi kuwa ukosefu wa virutubisho muhimu kama vile protini na vitamini utaendelea kusababisha wimbi kubwa la watoto wenye utapiamlo.
Makala hii imedadavua kwa kina, namna wazazi au walezi wanavyoweza kuepuka utapiamlo kwa watoto wao.
Maziwa ya mama yanaweza kuwa suluhu
Mtaalamu wa lishe kutoka Kituo cha Afya kilichopo Majohe jijini Dar es Salaam Blandina Cheyo, ameiambia Nukta Habari kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto walio chini ya miezi sita huzuia utapiamlo.
“Watoto wachanga wanatakiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita mfululizo ili kuzuia utapiamlo kwani maziwa ya mama yanavirutubisho vyote mtoto anavyo hitaji katika umri huu,” amesema Cheyo.
Vyakula vyenye virutubisho ni muhimu
Cheyo ameongeza kuwa baada ya miezi sita mtoto anaweza kuanza kupewa vyakula vyenye virutubisho kama wanga na madini huku akiendelea kunyonyweshwa hadi atakapofikisha miaka miwili.
Kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji huduma ya lishe kwa watoto wadogo ulioandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) mtoto anatakiwa apate angalau makundi mawili ya chakula kwenye kila mlo.
Makundi hayo ni pamoja na vyakula vya nafaka vinavyohusisha mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano, uwele viazi vikuu na ndizi
Aidha, vyakula vya jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama ikiwemo kunde, karanga, soya,nyama, samaki, dagaa, maziwa, na mayai vinashauriwa kutumika.
Malezi bora kwa mtoto
Pamoja na wazazi kutoa malezi bora kwa watoto mwongozo wa TFNC unashauri matumizi ya mbinu shirikishi kulisha watoto hususani wenye umri wa kuanzia miezi sita ili kuhakikisha wanapata chakula chenye virutubisho vya kutosha kwa wakati.