Mauzo ya parachichi yapaa kwa miaka mitatu mfululizo

Na Lucy Samson
11 May 2024
Uzalishaji wa zao la parachichi zinazouzwa nje ya nchi (exportable varieties) umeongezeka kutoka tani 17,711 mwaka 2021/22 hadi tani 26,826. mwaka 2022/23, ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa soko la ndani na nje ya nchi.
article
  • Mauzo yapaa mfululizo tangu 2020/21.
  • Kuimarika kwa soko nje ya nchi kwachangia. 
  • Wizara yajipanga kuongeza uzalishaji hadi tani 3,000.

Mauzo ya zao la parachichi nje ya nchi yamepaa kwa miaka mitatu mfululizo hadi kufikia Sh189.9 bilioni kwa mwaka 2022/23, jambo linalofungua fursa kwa Watanzania kuongeza uzalishaji na kufaidika na soko la kimataifa la mazao hayo.

Mauzo hayo yameongezeka kwa asilimia 61.6 kutoka Sh117.5 bilioni zilizorekodiwa mwaka 2021/22.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma Mei 2, 2024 amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa soko la zao hilo. 

“Uzalishaji wa zao la parachichi zinazouzwa nje ya nchi (exportable varieties) umeongezeka kutoka tani 17,711 mwaka 2021/22 hadi tani 26,826. mwaka 2022/23, ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Bashe.

Mauzo ya zao hilo yamekuwa yakiongezeka mfululizo tangu mwaka 2020/21 ambapo Wizara ya Kilimo imesema mwaka huo tani 15,432 za parachichi zenye thamani ya Sh102.1 bilioni ziliuzwa.

Wakati mauzo ya parachichi yakipaa, mauzo ya matunda mengine ikiwemo  chungwa, zabibu, nanasi, ndizi na embe yameongezeka hadi kufikia Sh347.3 bilioni kutoka Sh262.3 bilioni iliyokusanywa mwaka 2021/22.

Mazao mengine yaliyofanya vizuri katika mauzo ya nje ya nchi 2022/23 ni ndizi ambapo Sh113.7 bilioni zilikusanywa na chungwa lilioingiza Sh6.2 bilioni.

Ongezeko hilo la mauzo ya parachichi na matunda mengine linakuja wakati kukiwa na juhudi mbalimbali za Serikali kupanua masoko nje ya nchi ili kuwapatia wakulima soko la uhakika ili kujipatia fedha za kuboresha maisha yao.

Mwaka 2022 aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Anthony Mavunde alisema Tanzania imeshapata soko la matunda ikiwemo parachichi nchini China, Hispania na Afrika Kusini na kwamba wakulima wangeanza kusafirisha bidhaa zao za mazao hayo. 

Naye Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani mkoani Iringa Agosti 11, 2022 aliwaambia wananchi wa mkoa huo kuwa Serikali itajenga kiwanda cha kuchakata zao la parachichi ili kuyaongezea thamani mazao hayo kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

“Najua Iringa na Njombe ni wakulima wa maparachichi, kile kiwanda ambacho mbunge aliomba kisimamishwe kinabaki hapa. Na kule Njombe wameomba cha kwao tutawajengea,” alisema Rais Samia. 

Serikali kuongeza uzalishaji wa parachichi

Waziri Bashe aliwamabia wabunge kuwa wizara yake inatarajia kuongeza uzalishaji wa mazao ya parachichi hadi tani 3,000 kwa mwaka.

Ili kufikia malengo hayo wizara yake itashirikiana na wadau kuzalisha miche milioni 6 ya parachichi na kusambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.

Mipango mwingine ni kuwachimbia visima wakulima wa parachichi na kuwawekea miundombinu ya umwagiliaji na kuwapatia vifaa vya umwagiliaji kama vile pampu za maji na kutoa mafunzo.

“Tutatoa  mafunzo kwa wazalishaji wa miche 450, wakulima 4,000 na Maafisa ugani 160 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Kagera, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Morogoro pamoja na kutoa ruzuku ya viuatilifu kwa wakulima,” amesema Bashe.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa