Namna ya kupunguza gharama za manunuzi ya vyakula, vinywaji msimu wa sikukuu

Na Lucy Samson
18 Dec 2023
Mbinu zifuatazo zitakusaidia kupunguza gharama za maisha na mfumuko wa bei katika sikukuu za mwisho wa mwaka yaani Krismas na Mwaka Mpya.
article
  • Mbinu ya kwanza ni kupanga bajeti ya mahitaji ya chakula na vinywaji mapema.
  • Mbinu nyingine ni kununua mahitaji mapema na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima. 

 “Kila msimu wa sikukuu ukifika najua kabisa ndio wakati wangu wa kutoa fedha zaidi za matumizi ya nyumbani,” anaeleza Amani Barungwa, baba wa watoto watano.

Nusu ya mshahara wa Disemba wa Barungwa, mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, huishia kwenye manunuzi ya chakula na vinywaji kwenye msimu wa sikukuu za kila mwaka. 

Si Barungwa tu anayekutana na changamoto hiyo ya kutumia gharama kubwa kununua chakula na vinywaji, watu wengi nchini hapa hukutana na changamoto hiyo hususani wenye familia kiasi cha kupeleka maumivu zaidi Januari.

Hali ni  mbaya zaidi mwaka huu ambapo gharama za maisha na bei za bidhaa za vyakula zimeongezeka zaidi pengine kuliko miaka mingine.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka unaoishia mwezi Novemba, 2023 umefikia asilimia 3.7 kutoka asilimia 4.5 iliyorekodiwakwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2023

Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Novemba, 2023 umeongezeka hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 2.6 iliyorekodiwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2023.

Kutokana na kupanda kwa gharama hizo mbinu zifuatazo zitakusaidia kupunguza gharama huku mkifurahia sikukuu za mwisho wa mwaka yaani Krismas na Mwaka Mpya.

Wakati wa sikukuu, wafanyabiashara hupandisha bei ya vyakula, hivyo nunua mapema bidhaa zako. Picha| Daudi Mbapani.

Panga bajeti ya mahitaji ya muhimu mapema

Kwa kuwa sherehe nyingi za mwisho wa mwaka huambatana na chakula na vinywaji, hatua ya kwanza itakayokusaidia kupunguza matumizi ya pesa ni kupanga aina ya milo, vinywaji, pamoja na gharama zitakazohitajika.

Kwa mujibu  wa tovuti ya Ratesdotca kupanga bajeti na orodha ya chakula na vinywaji kunasaidia kutunza fedha na kuepuka kusahau baadhi ya mahitaji.

“Orodha haitaweka tu matumizi yako kwenye ufuatiliaji, pia inatumika kama ukumbusho mzuri ili usisahau bidhaa yoyote, jambo linalopunguza matumizi ya fedha ya ziada kununua bidhaa zilizosahaulika,” inasema tovuti hiyo.

Fanya manunuzi ya bidhaa za jumla

Ikiwa una familia kubwa yenye zaidi ya watu watano au unatarajia kupokea wageni msimu wa sikukuu, kununua bidhaa kwa bei ya jumla kunaweza kupunguza gharama za chakula na vinywaji  kwa kiasi kikubwa.

Mfano, bidhaa muhimu kama mchele ambayo baadhi ya maduka hutoa punguzo la bei ikiwa utanunua kwa bei ya jumla.

“Mchele ambao huuzwa Sh3,000 kwa bei ya rejareja unaweza kuuziwa Sh2,800 mpaka Sh2,500 kutegemea na wingi wa kilo utakazochukua,” amesema Shakur Issa, mmoja wa wauzaji wa mchele kwenye soko la Mwananyamala jijini Dar es Salaam. 

Siyo chakula tu hata bei ya vinywaji vya jumla ni tofauti kabisa na ile unayonunua rejareja ambayo hutoboa mfuko wako zaidi.

“Kreti moja la Soda linauzwa Sh12,000 mpaka Sh14,000 kwa bei ya jumla, ikiwa mtu akitaka rejareja itamlazimu kutoa Sh16,000 hadi Sh17,000 kununua soda 24 sawa na zile za kwenye kreti,” anasema Azory Ngajiro muuzaji wa vinywaji jumla jijini Dar es Salaam.

Pia soda kubwa za kopo ni njia nyingine nzuri ya kupunguza gharama za vinywaji, mfano soda moja kubwa ya kampuni ya Cocacola ya lita 2 inayouzwa Sh2,500 inaweza kutumiwa na watu watano mpaka sita.

Kwa njia hiyo unaweza kuokoa fedha ya ziada ambayo ingehitajika  kununua soda za mililita 350 zinazouzwa Sh600 au Sh700 kwenye  baadhi ya sehemu.

Ikiwa hupendelei soda unaweza pia kutengeneza juisi za matunda zisizohitaji kiasi kikubwa cha sukari na ukaokoa kiasi kikubwa zaidi cha fedha.

Unaweza kutumia mbinu hiyo hiyo pia iwapo unapendelea kupata pombe katika sikukuu yako. 

Kupanga bajeti ya vitu unavyovihitaji kwenye msimu huu wa sikukuu kunasaidia kuweka rekodi ya matumizi ya pesa yako. Picha | Daudi Mbapani.

Fanya manunuzi ya mahitaji mapema

Msimu wa sikukuu ndiyo kipindi ambacho baadhi ya wauzaji wa bidhaa hupandisha bei za chakula.

Kwa wauzaji hao kipindi hiki ni neema lakini kwa wanunuaji ni maumivu kwa kuwa hulazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kuweza kupata huduma hizo.

Ikiwa unatamani kupunguza gharama za chakula na vinywaji msimu huu wa sikukuu, mbinu ya kununua mapema inaweza kukusaidia kuokoa kiasi fulani cha fedha.

“Wauzaji wengi wa bidhaa wanakuwa hawajaanza kupandisha bei hivyo nunua kwa bei rahisi na uvitunze siku zikifika ni kupika tu,” anasema Atupele Mwakibasa aliyekuwa akipanga bidhaa zake kwenye gari baada ya kuzinunua kwenye soko la Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Mbinu hii inaweza kuwafaa zaidi wenye chumba maalum cha kutunzia bidhaa za chakula (store) au jokofu kwa bidhaa zinazoharibika kama nyama, matunda na mboga mboga.

Ikiwa hauna unaweza angalau kununua siku moja au mbili kabla ya siku ya sikukuu ili kuzuia zisiharibike.

Dhibiti manunuzi yasiyo ya lazima

Kwa baadhi ya watu msimu wa sikukuu ndicho kipindi cha kula na kusaza bila kujua kuwa mwisho wa msimu huu kuna mahitaji makubwa ya pesa ikiwemo kulipia ada za shule, kodi na gharama nyingine za msingi. 

Meshack Kimario, Mhasibu kutoka kampuni ya Inspire Consulting Firm anasema mbinu hii inamuwezesha mnunuzi kuyapa kipaumbele mahitaji muhimu huku ikimsaidia kutunza pesa.

Pia, mhasibu huyo anasema baadhi ya mahitaji yasiyokuwa ya lazima yanayonunuliwa sasa hivi huzuia manunuzi ya mahitaji mengine ya msingi zaidi.

 “Kuna watu wengi sana huko ambao hutumia gharama nyingi kwenye mahitaji ya chakula na vinywaji wakati wangeweza kuhifadhi pesa hizo zingeweza kutumika kwenye mahitaji mengine ya msingi au kutunisha akiba zao,” anasema Kimario.

Awali habari hii ilichapishwa katika tovuti ya Nukta Habari (www.nukta.co.tz)

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa