Serikali yaanika mikakati ya kupunguza gharama za nishati safi ya kupikia Tanzania

Na Lucy Samson
17 May 2024
Serikali ya Tanzania imeainisha mipango mikakati itakayosaidia kupunguza gharama ya nishati safi ya kupikia ili kuwezesha wananchi wengi kumudu gharama zake jambo litakalosaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama kama mkaa na kuni. Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliyekuwa akizungumza na wanahabari katika mkutano maalum ulioandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jijini Dar es […]
article
  • Ni pamoja na kuboresha miundombinu na kubuni teknolojia wezeshi.
  • Sh6.71 trilioni kuhamisha Tanzania kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Serikali ya Tanzania imeainisha mipango mikakati itakayosaidia kupunguza gharama ya nishati safi ya kupikia ili kuwezesha wananchi wengi kumudu gharama zake jambo litakalosaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama kama mkaa na kuni.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliyekuwa akizungumza na wanahabari katika mkutano maalum ulioandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jijini Dar es Salaam leo Mei 17, 2024 amesema mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya upokeaji wa gesi bandarini.

“Kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) tunayo mikakati ya kuboresha miundombinu ya upokeaji wa gesi bandarini tunaamini tukipokea gesi kwa kiasi kikubwa zaidi tutakuwa na mahusiano ya moja kwa mlaji,” amesema Kapinga.

Kauli hiyo ya Serikali kuhusu mikakati ya kupunguza gharama ya nishati safi kupikia inakuja wakati ambao wadau na wananchi wamekuwa wakilalamikia bei ya nishati hiyo kuwa juu jambo linalowafanya baadhi yao kushindwa kumudu na kutumia nishati nyingine zisizo salama.

Kapinga amesema ili kuwasaidia wananchi kumudu gharama za kwanza za manunuzi ya nishati hiyo Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilianza kutoa gesi bure katika baadhi ya maeneo na kwa sasa watasambaza gesi hizo kwa bei ya ruzuku.

Katika hatua nyingine Serikali imesema itaweka mkakati wa kuwashirikisha wadau kubuni teknolojia zitakazo wawezesha wananchi kumudu manunuzi ya gesi hizo kwa kuendana na vipato vyao.

Miongoni mwa wadau hao ni Kampuni ya M-Gas ambapo Mkuu wa Maendeleo na Ukuaji kutoka kampuni hiyo, Abdallah Kijangwa wakati akizungumza katika mkutano huo amesema wamebuni teknolojia itakayomuwezesha mwananchi kutumia kwa kadri ya mahitaji na uwezo alionao.

“Teknolojia yetu tunamuwezesha mtanzania kupata huduma ya gesi ya kilo 13 na mita janja itakayomuwezsha kunua gesi kwa Sh1,000, 500 mpaka Sh5,000…utakuwa unanua kama luku kiasi kile utakachoweza kulipia,” amesema Kijangwa.

Pia amesema kupitia ubunifu huo wananchi wataweza kununua gesi hiyo kwa bei ndogo na baadae kulipa kidogo kidogo kwa muda wa miaka mitatu jambo ambalo linaweza kuvutia wananchi wengi zaidi kuhamia katika nishati hiyo hasa wenye vipato duni.

Sh6.71 trilioni kuhamisha Tanzania kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Selemani Jafo, amesema ili kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030 Dola za Marekani bilioni 1.8 sawa Sh6.71 trilioni zinahitajika.

“Sisi Tanzania tuna fursa ukiacha huu mkakati wa pamoja kuna juhudi mbalimbali zinazohakikisha tunafanikiwa, hii ni kwa ajili ya Afrika na mkakati  wetu wa nchi ni Dola za Marekani bilioni 1.8,” amesema Waziri Jafo.

Kwa mujibu wa Jafo fedha hizo pia zitaisaidia Serikali kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi hususani wa vijijini.

Mbali na fedha hizo Jafo amesema tayari wadau wengine wameshaanza kuunga mkono jitihada za kuongeza matumizi ya nishati safi Tanzania wakiwemo Serikali ya Uingereza ambao wameahidi kutoa Dola za Marekani milioni 3.4 milioni sawa Sh8.82 trilioni.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa