Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaotumia sukari isiyo halisia, unapaswa kuchukua tahadhari kwa sababu zina madhara kwa afya yako.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo unaoshauri watu wasitumie vikoleza utamu visivyo sukari halisia (NSS) kwa lengo la kupunguza uzito na kuepusha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari.
WHO katika taarifa yake iliyotolewa Mei 15, 2023 Geneva, Uswisi inasema mwongozo huo umetolewa baada ya mapitio ya ushahidi unaodokeza kuwa kutumia sukari isiyo halisia kwa ajili ya kupunguza uzito hauna manufaa ya muda mrefu katika kupunguza mafuta mwilini miongoni mwa watoto na watu wazima.
Sukari hizo zisizo halisia na ambazo zinatumika ni pamoja na “aspartame, advantame, cyclamates, neotame, saccharin, sucralose na stevia.”
Kitu kibaya zaidi ambacho mapitio hayo yamebaini ni kwamba sukari hizo zisizo halisia zinaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2, magonjwa ya moyo na vifo miongoni mwa watu wazima.
Mkurugenzi wa WHO Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula Dk Francesco Branca amesema kuacha kutumia sukari ya kawaida kwa muda mrefu hakusaidii kupunguza uzito.
“Watu wanapaswa kufikiria njia mbadala za kupunguza matumizi ya sukari kwa kula vyakula vyenye sukari ya asili kama vile matunda au vinywaji na vyakula visivyo na sukari,” amesema Dk Branca.
Amesema vikoleza utamu visivyo na sukari havina lishe yoyote na kuongeza kuwa “watu wapunguze vyakula vitamu kwenye mlo wao tangu utotoni ili kuimarisha afya zao.”
WHO inasema pendekezo hilo linahusu watu wote isipokuwa wale wanaougua kisukari.
Mwongozo huo ni sehemu ya miongozo iliyopo na itakayotolewa ya lishe bora ambayo inalenga kuchagiza tabia nzuri za muda mrefu za ulaji wa vyakula zitakazosaidia kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza duniani.