Epuka vyakula, vinywaji hivi kulinda meno yako

Na Lucy Samson
24 Mar 2023
Pamoja kuwa na madhara ya kiafya ya jumla, vyakula vyenye sukari nyingi ni hatari kwa afya yako ya meno.
article
  • Ni pamoja na matunda yenye asidi kwa wingi na sukari ikiwemo peremende na ‘ice cream’.
  • Wataalamu wanashauri kula kwa kiasi.
  • Kusafisha meno mara kwa mara kunaweza kupunguza tatizo.

Dar es Salaam. Mara kadhaa nimekuwa nikiwasikia baadhi ya watu wangu wa karibu wakilalamika kuwa wanapata changamoto kwenye meno yao.

Baadhi yanawauma na baadhi meno yao yametoboka, jambo linalowasababishia maumivu au kushindwa kufurahia baadhi ya vyakula.

Inawezekana wewe au mtu wako wa karibu  ni miongoni mwao, lakini je unafahamu kuwa kile unachokula au kunywa kina athari ya moja kwa moja na afya ya meno yako?

Karibu katika makala haya ambayo yanaangazia vyakula vinavyopaswa kuepukwa ili kutunza afya ya meno yako, maoni haya ni kwa mujibu wa tovuti ya teknolojia ya nchini Marekani ya C-net pamoja na mahojiano na madaktari wa meno hapa jijini Dar es Salaam.

Vyakula vyenye sukari nyingi husababisha kuzalishwa kwa asidi inayoharibu utando wa juu ya meno na kusababisha meno kuoza.Picha|7News.

Matunda yenye asili ya asidi

Matunda haya ni miongoni mwa vyakula vinavyoathiri afya ya meno. Kama yakitumiwa kwa wingi, kemikali  iliyopo ndani ya matunda haya humomonyoa sehemu ya nje ya jino (enamel) na kurahisisha uvamizi wa vijidudu kwenda sehemu za ndani za jino.

Kwa mujibu wa Maktaba ya Matibabu ya Marekani (NIH),matunda kama machungwa, malimau, ndimu, zabibu huwa na Vitamini C ambayo ina kemikali iitwayo ‘ascorbic acid’ ambayo inaweza kuathiri tabaka la juu la jino kama itafikia kiwango cha ‘ph5.5’.

Wataalamu wanashauri kula matunda yenye asili ya asidi kwa kiasi  au kusukutua mdomo kwa  kutumia maji mara baada ya kumaliza kula aina hiyo ya matunda.

Vyakula vyenye sukari nyingi

Pamoja kuwa na madhara ya kiafya ya jumla, vyakula vyenye sukari nyingi ni hatari kwa afya yako ya meno. Vitu kama soda, peremende na keki huwa na sukari nyingi ambayo husababisha kuzalishwa kwa asidi.

Asidi hiyo ambayo hufanya kazi ya kuharibu tabaka la juu la jino  huzalishwa  pale mate yanapovunja vunja kemikali zilizopo kwenye vyakula hivyo kwa ajili ya kurahisisha mmeng’enyo. 

Kutokula kabisa vyakula hivi ndiyo njia bora ya kuepuka athari lakini kula kwa kiasi kunaweza kukupunguzia hatari ya meno yako kuharibika. Inashauriwa kutumia mrija pale unapokunywa vitu vyenye sukari nyingi ili kupunguza mgusano wa moja kwa moja kati ya vyakula hivi na meno yako.

Matunda kama machungwa huwa na kiwango kikubwa cha asidi hivyo inashauriwa kula kiasi. Picha l Esau Ng’umbi/ Nukta Africa

Barafu

Ndiyo, barafu ni hatari kwa afya ya meno yako. Inawezekana hujapenda kuiona katika orodha hii kwa sababu huwa unatafuna barafu mara kwa mara.

Iko hivi, kadiri unavyokula barafu ndivyo unavyozidi kuyahatarisha meno yako. Kwanza kutafuna barafu kunaweza kusababisha nyufa katika meno yako, lakini pia kama asidi na sukari barafu zinabomoa (enamel) gamba la juu la jino ambalo hufanya kazi ya kulinda jino.

Vyakula vya wanga

Kwa mujibu wa Dk Benard Yohana ambaye ni mtaalamu wa meno kutoka kliniki ya kinywa ya Ndovu iliyopo jijini Dar es Salaam, vyakula vya wanga kama mkate, tambi, na viazi vinaweza kuchangia kuoza kwa meno kwa sababu wanga unayojumuishwa kwenye vyakula hivi inaweza kubadilika kuwa sukari ndani ya kinywa.

“Ni muhimu kukumbuka kuwa vyakula hivi vinachangia kuoza kwa meno ikiwa vinaliwa mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa. Kwa hivyo, ni muhimu kula vyakula hivi kwa kiasi kidogo na kusafisha meno yako mara kwa mara. 

“Unaweza pia kujaribu kula vyakula vyenye protini, mboga za majani, na matunda ya mizizi kama vile karoti na viazi vitamu ambavyo vinaweza kusaidia kudumisha afya ya meno yako, “ anasema Dk Yohana.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa