Fahamu faida za kula magimbi kiafya

Na Mlelwa Kiwale
13 Aug 2024
Magimbi ni miongoni mwa vyakula vilivyopo katika kundi la mizizi ambalo kuna vyakula vingine kama viazi vitamu pamoja na mihogo. Katika baadhi ya maeneo chakula hiki huliwa sana wakati wa mfungo wa Ramadhani hivyo huwa ni nadra kuonekana wakati wote ingawa katika baadhi ya maeneo upatikanaji wake huwa wa muda wote hasa katika masoko rasmi. […]
article
  • Husaidia kuupa mwili nguvu na kuimarisha afya ya ubongo.
  • Inashauriwa kula kwa kiasi hususan kwa watu wanaoumwa kisukari.

Magimbi ni miongoni mwa vyakula vilivyopo katika kundi la mizizi ambalo kuna vyakula vingine kama viazi vitamu pamoja na mihogo.

Katika baadhi ya maeneo chakula hiki huliwa sana wakati wa mfungo wa Ramadhani hivyo huwa ni nadra kuonekana wakati wote ingawa katika baadhi ya maeneo upatikanaji wake huwa wa muda wote hasa katika masoko rasmi.

Licha ya kwamba hutumika kama kitafunwa wakati wa kifungua kinywa ambapo humenywa na kuchemshwa tu au katika upishi wa futari ambapo baadhi huyaunga nazi, magimbi yanatajwa kuwa na afya lukuki ambazo mlaji ananufaika nazo.

Makala hii imeangazia faida za kiafya azipatazo mtu anayekula magimbi kwa kurejea maoni ya wataalamu wa afya na lishe.

Huupa mwili nguvu

Magimbi yana madini ya kabohaireti yanayosaidia kuzalisha nishati na kuupa mwili nguvu hivyo yanaweza kutumika kama chanzo kizuri zaidi ya vyakula vya viwandani au vya kukaangwa na mafuta ambavyo havishauriwi sana na wataalamu wa afya.

John Bosco Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa amekuwa akijihisi kuwa na nguvu zaidi anapotumia magimbi kama kitafunwa tofauti na anapokula vyakula vingine kama maandazi au chapati.

“Nikila magimbi huwa nakuwa na nguvu tofauti na vitafunwa vyengine kama maandazi au chapati ambazo hunisababishia kupata njaa, kuliko magimbi ambayo huchukua muda mrefu,” amesema Bosco.

Kauli ya Bosco inaungwa mkono na Dk Stephe Mwenda mtaalamu wa lishe wa kujitegemea ambaye anabainisha kuwa vyakula vya jamii ya mizizi kama magimbi si tu husaidia kuupa nguvu mwili bali kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.

Aina ya virutubisho vinavyopatikana katika magimbi

Kwa mujibu wa Dk. Mwenda magimbi yamesheheni virutubisho lukuki kama vile Kalori, Protini, Nyuzinyuzi, Vitamini C, Vitamini B5, Manganizi’, Magneziamu, Potashiumu pamoja na Kopa ambavyo vina faida kiafya.

Kuimarisha afya ya ubongo

Mtaalamu huyo wa lishe ameongeza kuwa faida nyingine za magimbi ni pamoja na kuimarisha utendaji kazi wa ubongo, husaidia kupambana na baadhi ya saratani pamoja na kuimarisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Hata hivyo, Dk Mwenda ameshauri kuwa, ni muhimu kula chakula hicho kwa kiasi hususan kwa  watu wenye kisukari kwa kuwa husababisha kuongezeka kwa uzito.  

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa