Faida, namna ya kuandaa saladi ya matunda

Na Lucy Samson
17 Oct 2023
Kwenye makala hii utajifunza jinsi unavyoweza kuandaa saladi kwa gharama nafuu nyumbani kwako.
article
  • Utahitaji Sh3,000 kuandaa saladi ya watu wawili au watatu.
  • Tumia siki (vinegar) na ‘baking soda’ kusafishia matunda ili kuondoa wadudu

Saladi ni mchanganyiko wa matunda au mboga mboga ambao lengo lake ni kuongeza ladha kwa mlaji huku ikimpatia virutubisho mwilini.

Kwa mujibu wa tovuti ya Healthshots ulaji wa saladi humpatia mlaji mchanyiko wa virutubisho kama vile nyuzinyzui pamoja na aina mbalimbali za vitamini zenye uwezo wa kuimarisha afya ya mwili.

Hata hivyo, baadhi ya watu huwa hawatilii maanani sana umuhimu wake wanapoandaa au kununua chakula kwa kuwa hudhani ni kwa ajili ya watu fulani peke yake au huhofia bei yake.

Kwenye makala hii utajifunza jinsi unavyoweza kuandaa saladi kwa gharama nafuu nyumbani kwako.

Kikubwa kinachohitajika ni matunda kama embe lililoiva kiasi, nanasi, zabibu, ndizi, chungwa na limao ambayo unaweza kuyapata hata gengeni kwa ‘mpemba’.

Ikiwa unatamani kutengeneza saladi ya watu wawili au watatu, nikuhakikishie hautatumia zaidi ya Sh3,000 kuongeza saladi kwenye msosi wako.

Embe nunua la 500, nanasi nunua la 1,000 au vipande viwili vya 500, zabibu nunua za 500, ndizi nunua mbili kwa Sh500, inayobaki nunua chungwa moja na limao kwa Sh500 kisha tuelekee jikoni kuandaa.

‘Dressing’ husaidia kuongeza ladha kwenye saladi, unaweza ukaongeza viungo kadri upendavyo.Picha|love and lemons.

Jinsi ya kuandaa

Maandalizi ya saladi yanaanza kwa kumenya na kuosha matunda yote yatakayotumika.

Unaweza kutumia vinegar (siki) na baking soda au simba kama inavyotambulika na wengi ili yasafishike vizuri.

“Siki ni nzuri kwa kuondoa uchafu, inafaa sana katika kuua vijidudu vya kawaida vya jikoni na kupunguza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na chakula…

…pia ni chaguo salama kwani haina viungo vikali ambavyo vinaweza kuwa hatari kwa familia yako na mazingira,” inasema tovuti ya Garden Gate.

Anza kwa kukatakata embe na nanasi kwa saizi za pembe nne (cubes), ndizi zikate kwa umbo la duara na  zabibu unazoweza kuzikata kati au kuzitumia nzima nzima.

Unaweza kuandaa saladi nyingi au kidogo kiasi upendacho.Picha|She love biscotti.

Mpaka hapo unaweza kuwa umameliza, lakini utamu saladi unanogeshwa zaidi na ‘dressing’ (kimiminika kinachoongeza ladha katika saladi) ambayo leo tutaitengeneza kwa kutumia maji ya chungwa, limao, asali au sukari kiasi pamoja na chumvi.

Kwenye glasi au kikombe kamulia maji ya chungwa (unaweza kutumia chungwa moja au mawili kama hayana maji) na maji ya limao moja, ongeza vijiko viwili vya asali au sukari na chumvi robo kijiko  kisha koroga vichanganyike.

Baada ya hapo mimina ‘dressing’ yako katika saladi na uichanganye vizuri pamoja na matunda.

Katika hatua hiii wapo wanaopenda kuongeza mtindi na vanilla ili kuongeza utamu au saladi hiyo ya matunda.

Ikiwa umefanikiwa kufika hatua hii basi saladi yako itakuwa tayari kwa kuliwa, unaweza pia kuiweka kwenye friji ili ipoe na ‘dressing’ iweze kuingia vizuri.

Ikiwa hauna friji unaweza kuifaidi wakati wowote mara baada ya kumaliza kuitengeneza.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa