Jinsi ya kuhifadhi mananasi kwa kutumia mwanga wa jua

Na jikopoint
30 Sept 2023
Kikawaida huchukua muda wa siku mbili hadi nne kukauka kabisa ikiwa jua linawaka vizuri, na wakati mwingine muda unaweza ukawa mrefu zaidi kutegemeana na hali ya jua.
article
  • Mananasi yaliyokaushwa yanaweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miezi sita.
  • Hutumia siku tatu hadi tano kukauka, kutegemeana na mwanga wa jua uliopo.
  • Unaweza ukayatumia nyumbani au kwa biashara.

Ni utaratibu wa kawaida kwa baadhi watu ya kununua matunda mengi kwa ajili ya matumizi ya baadae, utaratibu ambao  husaidia kupunguza gharama za maisha na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.

Hata hivyo, wakati fulani changamoto inaweza ikawa namna ya kuyahifadhi, hususani kwa wale wasio na majokofu ambayo husaidia kutunza vyakula kwa muda mrefu zaidi.

Ikiwa nawe ni miongoni mwa wanaokabiliana na changamoto hiyo basi fuatilia makala hii hadi mwisho, ili ujifunze namna unavyoweza kuhifadhi tunda la nanasi kwa kutumia mwanga wa jua pekee.

Kwa mujibu wa tovuti ya ‘misosi’ mananasi yasiyomenywa yanaweza kukaa siku mbili hadi tatu na ukitaka yakae muda mrefu zaidi basi utalazimika kuyahifadhi kwenye jokofu ambapo yatakaa kwa siku 14.

Ikiwa umeyamenya, tovuti hiyo inashauri yawekwe kwenye jokofu ambapo yanaweza kudumu kwa siku saba pekee jambo linaloweza kuwa gumu kwa watu wanaotaka kuhifadhi tunda hilo kwa muda mrefu zaidi.

Hakikisha umeyatandaza mananasi kwa kuyapa nafasi ili yakauke kwa haraka.Picha|All Africa.

Hatua kwa hatua kukausha nanasi kwa kutumia jua

Hatua ya kwanza katika mbinu hii ya kuhifadhi nanasi kwa kukausha na jua  ni kuandaa mahitaji kama maji safi, chombo kikubwa cha kuoshea kifaa cha kufunikia (chenye matundu madogo madogo yasiyopitisha uchafu).

Pia utahitaji mananasi yasiyoiva sana, dawa ya kuhifadhi chakula (food preservative) unaweza kutumia ‘sodium metabisulphite’ inayopatikana  katika maduka ya chakula na dawa.

Ukimaliza kuandaa mahitaji,  anza kwa kuosha, kata vipande vidogo vidogo na uvianike juani mpaka vikauke sana, tumia nyavu yenye matundu madogo kuzuia uchafu kuingia.

Kikawaida huchukua muda wa siku mbili hadi nne kukauka kabisa ikiwa jua linawaka vizuri, na wakati mwingine muda unaweza ukawa mrefu zaidi kutegemeana na hali ya jua.

Baada ya mananasi kukauka yapitishe kweye dawa ya kuhifadhi chakula  (sodium ) ambapo utalazimika kuchanganya milimita 10 za dawa hiyo kwa kila lita moja ya maji.

Ikiwa unamatunda mengi zaidi pima lita kadhaa za maji kisha changanya na miligramu za dawa hiyo zinazondana na kiasi cha maji, ukimaliza  anika tena mananasi yakauke na yatakuwa tayari kuhifadhiwa kwa zaidi ya miezi sita.

Mbinu hiii pia inaweza kuwasaidia wajasiriamali wadogo wanaouza matunda kuhifadhi matunda na kuyauza kwa muda mrefu, pia wanaweza kusafirisha na kuwafikia wateja walio mbali.

Mbali na njia hii unaweza pia kukausha matunda hayo kwa kutumia vifaa vinavyokusanya miale ya jua kama jiko la sola ambalo hukausha kwa haraka zaidi.

Mbinu hii pia inaweza kuwa fursa kwa wajasiriamali kutengeneza na kusafirisha ndani na nje ya nchi.Picha|Home presserved.

Jinsi ya kutambua kama mananasi yamekauka

Kwa mujibu wa tovuti ya mkulima mbunifu mananasi yanaweza kuchukua sku tatu mpaka tano hadi kukauka kwa kiwango kinachotakiwa na ili kutambua kama yamekauka ni lazima yaweze kuvunjika kwa urahisi.

“Chukua kipande cha nanasi unachodhani kimekauka na kisha kikunje, mananasi yaliyokauka hukunjika kwa urahisi bila kukatika na hurudia katika umbo lake la awali yakikunjuliwa

Pia mananasi yaliyokauka hayatakiwi kuonyesha dalili za unyevu au kukatika yakikunjwa,” imesema tovuti hiyo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa