Jinsi ya kutambua tikiti maji lilioiva vizuri

Na Lucy Samson
8 Nov 2023
Leo nikufumbue macho kidogo ili ukienda sokoni mara nyingine usiingie mkenge wa kuchagua tikiti lisiloiva vizuri
article
  • Ni pamoja kupauka kwa rangi na kuwa na kikonyo kikavu.
  • Hutoa mlio mzito zaidi wa sauti likigongwa tofauti na bichi.

Huenda umeshawahi kununua tikiti halafu wakati wa kula ukagundua halikuwa limeiva vizuri na kujikuta umepoteza fedha, muda pamoja na kukosa vitamini muhimu.

Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa katika tovuti ya utafiti ya Research Gates, tikiti maji lisiloiva lina virutubisho vichache kulinganisha na lile liliova ambalo husheheni  protini, kashiamu,Vitamin A, B6, C, zinazofanya kazi mbalimbali ikiwemo kuondoa sumu mwilini na kuupa mwili uwezo wa kukabiliana na maradhi.

Leo nikufumbue macho kidogo ili ukienda sokoni mara nyingine usitumie muda mwingi kuchagua tikiti lililoiva, au kughairi kabisa kununua tunda hilo fanya yafuatayo ili kuepuka kuingia mkenge.

Chagua tikiti lililobadilika rangi kiasi

Kwa baadhi ya wajuvi wa mambo, wanafahamu tunda lolote likiiiva huwa na desturi ya kubadilisha rangi, jambo linalotumika kama ishara kwa walaji kuwa lipo tayari kwa kuliwa.

Christopher Lawrence, mkulima wa matikiti mkoani Arusha ameiambia JikoPoint kuwa tikiti lililoiva huwa linabadilika rangi kutoka kijani iliyokolea hadi kwenye kijani mpauko na rangi ya manjano iliyofifia kwa matikiti ya kisasa.

“Matikiti yakiwa yamekomaa yanabadilisha rangi badala ya kuwa kijani iliyokolea yanakuwa kijani mpauko, yani liende kwenye rangi fulani hivi inayofanana na njano iliyopauka,” amesema Christopher.

Tikiti maji ni iongoni mwa matunda yanayofaa kwa watu wa rika zote.Picha|Simly recipe

Mlio wa tofauti

Kwa upande wake Arnold Mkingimba, muuza matikiti jijini Dar es Salaam anasema tikiti lililokomaa vizuri, lenye ladha tamu huwa linatoa mlio wa tofauti pale utakapo lipiga.

“Tikiti lolote lililokomaa au lililoiva vizuri ukilipiga linakuwa na mlio wa touti, linalia kama mpira au kama umeweka kitu ndani…kutumia mbinu hii lazima uwe mzoefu hivi hivi huwezi kujua,” ameongeza Mkingimba.

Aidha, tovuti ya chakula ya Real Simple ya inasema tikiti lililoiva vizuri likigongwa kidogo hutoa mlio mzito kiasi kulinganisha na lile lisilo iva vizuri ambalo hutoa mlio mwepesi.

Kikonyo kikavu

Mara nyingi matunda yaliyokomaa na kuiva vizuri vikonyo vyake huwa vimekauka, yakiashiria kuwa yalikaa muda mrefu shambani na yapo tayari kwa kuliwa huku yakiwa na utamu wa kutosha.

“Siku hizi kuna wale wanaovundika matunda, unakuta tunda ni kubwa lakini halijaiva vizuri wao wanalichukua na kuja kuuza, kama ni mjanja ukiona  tu kikonyo ni kibichi unajua ni bichi ,” anasema Mkigimba.

Ukubwa na umbo la tikiti

Hapa ndipo penyewe, kuna baadhi ya watu wao hupenda kukimbilia matunda makubwa bila kuzingatia vigezo vingine vinavyoyafanya yawe bora.

Mara zote hakikisha unachagua tikiti lenye umbo la duara, wauzaji wa tikiti wanasema matikiti yenye umbo hilo ndiyo yanaongoza kwa kupendwa na walaji kwani ni matamu.

Kuhusu uwepo wa matikiti  yenye maumbo nyingine Christopher anasema ni vyema kuzingatia vigezo vingine ikiwemo mlio, uwepo wa kikonnyo kikavu na kubadilika kwa rangi.

Mbali na tikiti maji kuliwa kama tunda, linaweza kutoa juisi tamu ikiwa likichanganywa na matunda mengine.Picha|Juixe and Lemon

Omba kukatiwa kipande

Kwa baadhi ya wauzaji hukubali kukata kipande kidogo kwenye tikiti alilochagua mteja ili ajiridhishe kama chaguo lake lipo sawa au la.

Njia hii inaweza kukupa uhakika wa tunda lako angalau kwa asilimia 50, kwa kuwa unakuwa umeona kiasi cha uivaji wake.

Hata hivyo, si wauzaji wote wa matikiti hukubali njia hii, unaweza kutumia njia nyingine au kwenda kwa muuzaji mwingine atayekubali kufanya hivyo.

Mambo ya kuzingatia

Pamoja na vigezo vyote hivi vinavyoweza kubainisha tikiti lililokomaa na kuiva vizuri ni vyema kuzingatia muonekano wa nje wa tunda lako, hakikisha halina mipasuko au mabaka baka yanayoashiria kuharibika au kukaa sana sokoni.

Pia unaweza kunusa tikitiki lako mara kadhaa kuhakikisha halijaoza, ni salama kwa kula ili kujiepusha kupata magonjwa ya tumbo yatokanayo na kula vyakula  vilivyoharibika.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa