Usifanye makosa haya wakati wa kununua blenda

Na Rodgers George
27 Sept 2022
Hakikisha unafahamu matumizi yako, vitu unavyoenda kusaga, bei na ubora wa kifaa unachonunua.
article
  • Hakikisha unafahamu matumizi yako na aina ya vitu utakavyotengeza.
  • Ukubwa na ubora wa blenda nao uzingatiwe.
  • Kama hujui ni vema kuuliza kwa wataalam wa kueleweshe kuhusu blenda inayokufaa.

Mara nyingi, watu hununua kitu kwa sababu kinakidhi mahitaji yao bila kufahamu kuwa kila kitu kimetengenezwa kwa ajili ya kutimiza kusudi fulani ambalo linaweza lisishabiane na kusudi lako.

Kama sentensi hiyo inavyochanganya, ndivyo watu wengi hujikuta wakiwa kwenye sintofahamu baada ya kununua kitu dukani na kitu hicho kukaa kwa muda fulani na kisha kuharibika.

Kwa leo, tuangazie kwenye manunuzi ya mashine ya kutengenezea juisi maarufu kwa kimombo kama “Blender”.

“Kuna blenda ambazo wenyewe wanaziita ni commercial (za matumizi ya biashara) ambazo zinakuwa zimeundwa kwa jili ya vitu vigumu. Muundo wake unakuwa imara zaidi,” amesema Googluck Paul ambaye ni muuzaji wa vitu vya umeme jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa mashine hii, hawalijui hilo, wengi ilimradi inatengeneza juisi watakavyo na bei yake inaeleweka hilo linatosha.

Wasichokijua ni kuwa kwa kutumia blenda ambayo siyo sahihi kwa matumizi yao, huenda wakaingia gharama nyingi zikiwemo za kununua blenda mpya au kutumia umeme mwingi na kuwaongezea gharama za maisha.

Uzingatie nini wakati unanunua blenda yako?

Matumizi yako

Grace Mlimakala ni muuzaji wa juisi mkoani Shinyaga amesema hutengeneza lita tano hadi sita kwa siku kwa ajili ya wateja wake.

Hata hivyo, Grace amesema blenda anayoitumia inatengeneza juisi lita moja kwa wakati moja na hivyo kulazimika kuandaa juisi mara sita illi kukamilisha kazi yake.

Kwa mfanyabiashara kama Grace, angeweza kununua blenda kubwa ya lita mbili na kusaga juice hiyo mara tatu tu hivyo kurahisisha kazi zake na huenda kupunguza gharama za umeme.

“Matumizi ya umeme yamebadilika. Yameongezeka kutoka uniti tatu na sasa natumia uniti saba kwa siku,” amesema Grace akielezea hali ya matumizi ya umeme kabla na baada ya kuanza kuuza sharubati.

Kabla ya kununua mashine hiyo, tafakari kwanza mahitaji yako ili ununue ile inayokufaa.

Blenda ni kifaa muhimu kwa shughuli za kutengeneza bidhaa mbalimbali za nyumbani ikiwemo juisi. Picha | Pampered Chef.

Aina ya vitu vya kutengeneza

Meneja wa mgahawa wa juisi wa Daily Juice uliopo Mbezi beach karibu na kanisa la KKKT jijini Dar es Sallaam, Neema Titus amesema blenda hutofautiana kutokana na vitu unavyovisaga.

“Kuna Blenda ya kutengenezea juisi ambayo inahitaji uweke maji ili ifanye kazi vizuri, zipo ambazo zinaweza kusaga hadi mabonge ya barafu na zipo mashine za kusaga juisi ambazo husaga chochote bila haja ya maji,” amesema meneja huyo.

Wataalam wa vifaa vya kielektoniki akiwemo Paul wanasema kila mashine ina uwezo wake wa matumizi ya umeme, kwahiyo ni vema kutathmini aina ya vitu unavyotaka kutengeneza kwenye blenda.

Fahamu watu watakaoitumia

Kama unanunua blenda kwa ajili  yamatumizi ya nyumbani, hakikisha unatafuta blenda itakayohimili watu hao. Hauna haja ya kununua blenda yenye jagi la kioo kama unafahamu kuwa watoto wanaweza kuitumia.

Kwa kuzingatia hilo, unaweza kujiepusha na gharamma za kutafuta jagi lingine pale la kwanza linapovunjika.

Bei na ubora wa blenda

Kuna blenda nyingi sokoni. Zipo za hadi Sh65,000 lakini kwa mujibu wa Caroline Kabogo, ambaye alinunua blenda kwa bei hiyo, haikudumu muda mrefu. 

Tofauti na Kabogo, Neema amesema alinunua blenda mwaka 2017 iliyogharimu Sh250,000 na anaitumia hadi leo na iko bomba.

Hata hivyo, bei siyo kigezo sahihi cha kupima ubora wa blenda, licha ya kuwa baadhi ya watu hutengeneza vifaa hivyo visivyo na ubora na kuviuza kwa bei ya chini. 

Kwa kuzingatia hayo, unaweza kuepuka makosa wakati wa kununua blenda ili kuipata ile inayoendana na mfuko wako, mahitaji yako huku ikiwa bora na kudumu kwa muda mrefu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa