Faida, jinsi ya kutengeneza ‘milkshake’ ya parachichi

Na Lucy Samson
9 Sept 2023
Parachichi lina wingi wa madini ya potasiamu hivyo linaweza kudhibiti shinikizo la damu na kufanya mapigo ya moyo kuwa ya kawaida.
article
  • Ina wingi wa virutubisho vinavyoimarisha kinga ya mwili.
  • Ni rahisi na haichukui mda mrefu.

Parachichi ni moja ya tunda pendwa na linalopatikana kwa wingi katika maeneo mengi Tanzania, na ni tunda ambalo hutumika kusindikiza mlo wowote iwe ni asubuhi, mchana au jioni. 

Tunda hilo pia hutumiwa kutengeneza saladi, kupamba sahani na kutengeneza aina mbalimbali za juisi ikiwemo milkshake ya parachichi inayotengenezwa kutokana nkwa kuchanganywa na maziwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya ‘PharmEasy’ juisi ya parachichi ina wingi wa virutubisho vyeye uwezo mkubwa wa kupunguza athari ya magonjwa ya muda mrefu (chronic diseases) mwilini.

“Parachichi lina wingi wa madini ya potasiamu hivyo linaweza kudhibiti shinikizo la damu na kufanya mapigo ya moyo kuwa ya kawaida,” imesema tovuti hiyo.

Hata hivyo, tovuti hiyo imeshauri kufuata ushauri wa daktari ikiwa unataka kutumia parachichi kama tiba.

Hakikisha umeweka maziwa ya kutosha kwenye blenda ili kuwezesha parachichi kusagika vizuri.Picha|Tummy to Heart.

Mbali na parachichi maziwa ambayo yanatumiwa katika kinywaji hiki yana faida nyingi katika mwili wa binadamu ikiwemo kuimarisha afya ya mifupa.

Kutokana na faida hizo kuna kila sababu ya kujifunza kuandaa kinywaji hiki kwa ajili yako, familia yako au hata wateja unaowahudumia.

Maandalizi ndani ya dakika 10

Tofauti na aina nyingine za juisi, milkshake ya parachichi huandaliwa kwa muda mfupi usiozidi dakika 10 ikiwa unatengeneza juisi ya kunywa watu wawili au watatu.

Hatua ya kwanza ya maandalizi ni kuchemsha maziwa ya ng’ombe, na ikiwa utatumia maziwa ya boksi ya kununua dukani basi haina haja ya kuchemsha.

Kama hautumii maziwa ya ng’ombe hiyo siyo sababu ya kushindwa kutengeneza kinywaji hiki, unaweza kuweka maziwa ya lozi (almondi) na korosho.

Maziwa ya almondi na korosho hupatikana madukani, ila unaweza kutengeneza nyumbani kwa kuziloweka kwa masaa 12 au zaidi kisha kuzisaga pamoja na maji.

Ukimaliza kuchemsha maziwa anza kuandaa maparachichi kwa kuyamenya na kuyakata vipande vidogo, kisha mimina kwenye blenda pamoja na maziwa.

Baada ya hapo saga kwa pamoja kwa muda wa dakika mbili au tatu kisha utaangalia kama mchanganyiko wako umesagika vizuri na kuwa laini.

Kumbuka ‘milkshake’ haichujwi hivyo saga kwa muda mrefu iwezekanavyo  ili kupata mchanganyiko unaoweza kuunywa bila kuchuja.

Ongeza sukari kiasi au asali kama unapendelea kisha milkshake yako itakuwa tayari kwa kunywa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa