Jinsi ya  kutoa sumu mwilini kwa kutumia chungwa na tangawizi

Na Lucy Samson
5 Jun 2023
Virutubisho vilivyopo kwenye chungwa na matunda mengine yenye uchachu kama ndimu na limao, husaidia ini kufanya kazi yake vyema, pamoja na kusaidia kuondoa seli zilizokufa mwilini.
article
  • Ni kwasababu  vyakula hivyo vina virutubisho vinavyochochea sumu kutoka haraka na kuimarisha kinga ya mwili
  • Unaweza kutengeneza kwa kutumia mashine ya umeme au kwa mikono

Chakula ni miongoni mwa mahitaji ya msingi kwa binadamu kwa kuwa  husaidia katika uzalishaji wa nishati inayotuwezesha kufanya shughuli mbalimbali.

Hata hivyo wakati fulani chakula huwa ni sehemu ya tiba katika kuuponya mwili kutokana na baadhi ya vyakula kuwa na virutubisho ambavyo vinaweza kuponya na kuukinga mwili na aina ya virusi au bakteria.

Huenda umekuwa ukila machungwa kama kiburudisho tu na ukiitumia  tangawizi kama kiungo cha chai au chakula  lakini hujui kama vitu hivyo vikichanganywa pamoja unaweza kupata tiba nzuri inayosaidia kupunguza sumu mwilini.

Nukta habari imefanya utafiti katika tovuti mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya afya na kukuandalia makaa ifuatayo inayofafanua kwa undani namna unavyoweza kuondoa sumu mwilini kwa kutumia machungwa na tangawizi.

Kwanini machungwa

Machungwa ni miongoni mwa matunda yaliyo kwenye kundi la matunda yenye uchachu, uchachu huo husababishwa na kusheheni kwa kirutubisho cha vitamin C ambayo huwa katika mfumo wa alkali.

Kwa mujibu wa tovuti ya  afya ya Hindustan Times ya  nchini India, Alkali hiyo husaidia kuimarisha kinga ya mwili pamoja na kusawazisha uwiano wa asidi mwilini.

Virutubisho vilivyopo kwenye chungwa na matunda mengine yenye uchachu kama ndimu na limao, husaidia ini kufanya kazi yake vyema, pamoja na kusaidia kuondoa seli zilizokufa mwilini.Picha|iStock.

Daktari Nivedita Pandey katika blogu yake ya masuala ya afya amesema juisi ya chungwa  ina kiasi kikubwa cha vitamini C na potasiamu ambayo hulinda seli za ini kutokana na sumu. 

Sambamba na faida hizo za kiafya tovuti ya BBC good food inasema aina hii ya juisi inaweza pia kusaidia kupunguza uzito endapo  mtumiaji atajihusisha na shughuli nyingine hususan kufanya mazoezi.

Maajabu ya tangawizi

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tangawizi ni mmea wenye asili ya mzizi ambao upo kundi moja na mimea mingine kama manjano ambapo asili yake ni Asia ya Kusini-Mashariki, India na China.

Mmea huu umezoeleka kutumika kama kiungo cha chai ama chakula kakini BBC wanabainisha kwamba gramu 10 tu za tangawizi hutoa gramu mbili za protini

gramu moja ya lipids, gramu nane za wanga, gramu mbili za nyuzinyuzi pamoja na miligramu 42 mg za potasiamu.

Mkusanyiko huo wa virutubisho hufanya kazi mbalimbali mwilini ikiwemo kusaidia mmeng’enyo wa chakula, kuimarisha mifumo ya utoaji taka mwilini kama jasho na njia ya mkojo, kuzuia kichefuchefu pamoja na kuzuia damu kuganda katika mishipa ya damu.

Ni wazi kuwa mchanganyiko wa machungwa na tangawizi unaweza kukusaidia kuimarisha afya ya mwili wako na kupunguza sumu zilizopo mwilili kutokana na namna virutubisho vyake vinavyofanya kazi mwilini.

Maandalizi

Nunua machungwa matatu(unaweza kuongeza kama unatengeneza juisi kwa ajili ya familia) na tangawizi kiasi kisha uyamenye baada ya hapo 

yakate na  uyaweke kwenye bakuli safi kisha andaa mashine ya kutengenezea sharubati yako.

Baada ya hapo changanya machungwa na tangawizi na maji kiasi kisha usage mpaka yalainike.

Ukimaliza chuja, weka katika chombo kisafi ongeza barafu, sukari kiasi au asali kwa matokeo mazuri zaidi.

Ikiwa hauna mashine ya umeme  unaweza kutumi ya mkono  au ukayakamua vizuri na kuchuja mbegu na nyuzi nyuzi kisha ukachanganya na tangawizi ambayo unaweza kuitwanga au kuikuna na baada ya hatua hizo kinywaji chako kitakuwa tayari kwa kunywa

Je wewe unatumia njia gani kupunguza sumu mwilini?

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa