Uzingatie nini unapotengeneza ‘Yogurt’?

Na Lucy Samson
22 Feb 2023
Yogurt ni kinywaji chenye wingi wa protini na madini chuma kinachotengenezwa kwa maziwa kikinakshiwa kwa ladha mbalimbali ikiwemo vanila,
article
  • Yogurt ni moja ya vinywaji vyenye wingi wa protini na madini chuma.
  • Unaweza kutengeneza nyumbani kwa mahitaji machache.

Ukitaja jina ‘Yogurt’ taswira ya haraka itakayowajia wengi kichwani ni kinywaji cha kuburudisha na utamu wa aina yake hususani kikiwa cha baridi.

Kwa wasiofahamu Yogurt ni kinywaji chenye wingi wa protini na madini chuma kinachotengenezwa kwa maziwa huku kikinakshiwa kwa ladha mbalimbali ikiwemo vanila, nanasi, embe, au Strobeli (strawberry).

Kutokana na utamu wake watu wengi wamekuwa wakitamani kujua mbinu za kutengeneza nyumbani ili waweze kuepuka kutoboa mifuko yao zaidi kununua kinywaji hicho madukani.

Jikopoint (www.jikopoint.co.tz)  imekuletea maujanja ya kutengeneza kinywaji hiki kwa mahitaji machache tu:

Maandalizi

Hatua ya kwanza ni kuandaa jiko kwa ajili ya kuchemsha maziwa.

Andaa sufuria, hakikisha sufuria ni safi na kavu kisha mimina maziwa na uache mpaka yaive kwa dakika tano au zaidi.

Maziwa yanayotumika kutengeneza kinywaji hiki  ni ya ng’ombe na wala siyo ya kutoka viwandani yanayouzwa madukani. Hakikisha haufuniki sufuria unayochemshia maziwa, kufunika kunaweza kusababisha yogurt yako iwe chungu mwishoni.

Baada ya maziwa kuchemka ipua na umimine kwenye chombo kisafi kisha uache yapoe, kisha mimina nusu kikombe cha yogurt ya dukani isiyo na ladha kisha ukoroge vizuri ichanganyike na maziwa.

Baada ya hapo yafunike kwa mfuniko usiopitisha hewa kwa saa 6 au zaidi kisha yogurt yako itakuwa tayari ikiwa hupendelei ladha wala sukari.

Unaweza kugandisha Yogurt kwenye friji kwa masaa manne mpaka sita ili kuendelea kufurahia zaidi kinywaji hiki.Picha|Living Health

Tuweke ladha na sukari

Gawa yogurt yako kwenye mabakuli tofauti ikiwa utapendelea kuweka ladha zaidi ya moja. Kama ukitaka ladha moja basi tumia bakuli hilo hilo la mwanzo.

Mimina kiasi cha sukari na ladha kiasi kisha ukoroge ichanganyike vizuri.

Ukiridhika na kiasi cha ladha na sukari uliyoweka, weka yogurt yako kwenye friji au ongeza vipande vya barafu na kinywaji chako kitakuwa tayari.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa