Fahamu aina za mchele na mapishi yake

Na Fatuma Hussein
26 Feb 2025
Jiko point imekusogezea aina za mchele unazoweza kutumia kuandaa mapishi mbalimbali iwe nyumbani au katika sherehe.
article
  • Ni pamoja na mchele mweupe, basmati na jasmini.

Mchele ni miongoni mwa vyakula pendwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kikitumika kama sehemu ya mlo katika sherehe na hafla mbalimbali zinazohitaji msosi.

Si shughulini pekee hata majumbani mchele hupikwa kwa mapishi ya aina mbalimbali ili kuvutia walaji wake.

Kama wasemavyo waswahili mchele mmoja mapishi mbalimbali ndivyo ilivyo kwa nafaka hii ambayo ina uwezo wa kuandaa aina mbalimbali za misosi kulingana na aina ya mchele utakaotumia.

Jiko point imekusogezea aina za mchele unazoweza kutumia kuandaa mapishi mbalimbali iwe nyumbani au katika sherehe.

Mchele mweupe
Mchele mweupe ni aina ya mchele ambayo unatokana na zao la mpunga ambao hukobolewa ili kuondolewa ganda la nje kubakisha nafaka safi nyeupe.  

Hata hivyo, mchele huu unapokobolewa, hupoteza baadhi ya virutubisho muhimu vinavyohitajika katika mwili wa binadamu. 

Mchele mweupe hutumika katika mapishi mengi, kama vile pilau, wali wa maua, mkate wa mchele, mseto wa wali, kupika wali wa karoti na hoho na mapishi mengine rahisi ya wali.

Mchele wa kahawia
Huu ni mchele wa asili ambao haujasafishwa sana, hivyo una ganda na kiini. 

Ni mchele wenye virutubishi vingi na unachukua muda mrefu zaidi kupika.

Mchele wa kahawia ni mchele ambao haujakobolewa kabisa, hivyo unahifadhi nyuzi na virutubisho vyake kama vile vitamini na madini. 

Mchele huu ni mzito kidogo kuliko mchele mweupe na una ladha yenye utamu wa asili. 

Aina hi hya mchele huwafaa zaidi wagonjwa wa kisukari na hutumika kutengeneza mapishi kama mkate, vitumbua na vyakula vingine vinavyohitaji mchele kama kiamba upishi kikuu.

Mchele wa kahawia una wingi wa nyuzi nyuzi na vioksidishaji vinavyoongeza virutubishi mwilini.Picha|Royal lee

Mchele wa basmati
Mchele huu wenye asili ya Asia na India ni miongoni mwa michele inayosifika kwa harufu nzuri na kuandaa chakula kitamu kinachovutia walaji.

Kwa kutumia mchele huu pia unaweza kupika mapishi kama wali wa limao,wali wa nazi ambao hupendelea zaidi kusini mwa India, wali wa kukaanga na mayai, ‘Tawa pulao’, ‘Paneer Pulao’, ‘Pav Bhaji’ ambavyo zote asili yake ni India.

Mchele mweusi

Mchele mweusi ni mojawapo ya aina maalumu na za hali ya juu za mchele unaozalishwa katika nchi za Afrika Mashariki.

Mbali na nchi za Afrika Mashariki mchele huu pia unazalishwa barani Asia ikiwemo katika nchi za Thailand, Japan, Ufilipino, Korea, India, China, Iran, Pakistan, India, Bangladesh na hata Afghanistan. 

Mchele mweusi unaweza kupikwa sawa na aina nyingine za wali, ingawa unaweza kuhitaji maji zaidi na muda mrefu wa kupika kutokana na umbile lake nene.

Mchele huu unaweza kuupika kwenye supu, au aina nyingine za chakula ikiwemo sushi.

Mchele wa jasmine
Mchele wa Jasmine ni mchele mwenye urefu na una harufu nzuri kama ya maua. 

Ni maarufu sana katika ya asili ya Asia ya Kusini Mashariki, na una harufu nzuri ya maharage.

 Mchele huu ni laini na una ladha tamu kidogo, na ni mzuri kwa mapishi ya vyakula vya Asia, hasa vyakula vya Thailand na Vietnam. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa