Parachichi ni miongoni mwa matunda maarufu nchini Tanzania na maeneo mengine duniani, hutumiwa na makundi mbalimbali ya watu kuanzia watoto hadi watu wazima.
Tunda hilo ambalo linajulikana kama Persea americana linatoka katika familia ya Lauraceae ni matunda yenye asili ya kutoka kusini, kati na Kaskazini mwa Amerika.
Pamoja na jamii hiyo, kuna jamii nyingine za parachichi ambazo zimeendelea kuzalishwa na kuenea katika nchi mbalimbali duniani kama Guatemala (Guatemalan race) na jamii ya India Magharibi (West Indian race).
Tanzania huzalisha wastani wa tani 190,000 za parachichi ambapo uzalishaji huu umechangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Taifa, ambapo thamani ya mauzo ya nje ya parachichi imeongezeka kutoka Sh14.9Â bilioni mwaka 2020 hadi Sh 25 bilioni mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwaka 2022 Tanzania iliuza nje takribani tani 18,993 za parachichi zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 22.1
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inabainisha kuwa kuna aina mbili za parachichi ambazo ni parachichi za asili na parachichi za kisasa/ chotara.
Aina hii ya parachichi inapatikana zaidi katika maeneo ya zamani ya kilimo cha parachichi nchini. Miti yake huwa mirefu, yenye majani mapana na shina imara.
Parachichi za asili huchukua muda mrefu kutoa maua na matunda, na mavuno yake kwa kawaida ni machache ukilinganisha na aina za kisasa.
Hata hivyo, matunda yake huwa makubwa, yenye ladha ya asili na kiwango cha chini cha mafuta.
Wakulima wengi huzipanda kwa matumizi ya nyumbani zaidi kuliko biashara, kutokana na changamoto za urefu wa miti na muda mrefu wa matunda kukomaa.
Aina hizi zimeboreshwa kisayansi kwa kuchanganya tabia bora za parachichi za asili kutoka maeneo tofauti ya Amerika.
Zina sifa ya kutoa matunda mengi, yenye ubora wa juu, kukomaa mapema na kuwa na mafuta mengi yenye afya na ndio maana wafanyabiashara wengi huyapendelea
Na hizi ndio baadhi ya aina maarufu za parachichi za kisasa zinazolimwa na kupendwa zaidi nchini Tanzania.
Hii ni aina maarufu duniani na inauzwa kwa wingi katika masoko ya kimataifa.
Tunda la Hass lina umbo la yai, ngozi yenye vipele vidogo na hubadilika rangi kutoka kijani kibichi hadi kahawia linapokomaa.
Hukomaa kati ya miezi 10 hadi 14 baada ya maua, hasa katika maeneo yenye baridi.

Uzito wa tunda ni kati ya gramu 150 hadi 300, na nyama yake ni laini, isiyo na nyuzi nyuzi, ikibeba mafuta bora yenye thamani ya asilimia 18 hadi 23.
Hass ina soko kubwa kutokana na ladha yake tamu, ubora wa kuhifadhiwa kwa muda mrefu na urahisi wa kusafirishwa.
Fuerte ni aina ya chotara iliyopatikana kutokana na kuchanganya aina za Guatemala na Mexico.
Ngozi yake ni nyembamba, laini na rahisi kumenya, jambo linaloifanya ipendwe sana na watumiaji.

Hukomaa ndani ya miezi 4 hadi 6 tangu maua kuchanua, na matunda yake huwa na uzito wa kati ya gramu 230 hadi 500.
Fuerte ina kiwango cha mafuta kinachofikia asilimia 16 hadi 25 na ladha yake ni laini, ikitambulika kama parachichi la ubora wa kati linalofaa zaidi kwa kula mbichi au kuchanganya katika saladi.
X-Ikulu ni aina inayotamba katika mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania kama Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma.
Tunda lake ni kubwa, lenye umbo linalofanana na tunda la embe, na ganda lake hubaki kijani hata baada ya kuiva.

Majani yake ni mapana, na mti wake ni imara wenye uwezo wa kustahimili baridi.
Aina hii hukomaa ndani ya miezi sita baada ya maua na hupatikana sokoni katika kipindi ambacho aina nyingine hazijakomaa, hivyo kuongeza thamani yake kibiashara.
Parachichi la Pinkerton linafanana kwa sura na aina ya hass, lakini lina shingo ndefu zaidi.
Ngozi yake ina vipele vidogo na hubaki kuwa na rangi ya kijani hata baada ya tunda kukomaa.
Uzito wake ni kati ya gramu 270 hadi 400, na kiwango cha mafuta ni asilimia 18 hadi 25.

Nyama ya ndani ni laini, yenye ladha tamu na isiyo na nyuzinyuzi, hivyo kuifanya kuwa chaguo bora kwa wapenzi wa juisi na saladi za matunda.
Nabal ni parachichi lenye umbo la mviringo na rangi ya kijani kibichi inayong’aa. Linalimwa zaidi katika maeneo ya wastani wa joto.
Uzito wa tunda hili ni kati ya gramu 300 hadi 500, na lina ngozi ngumu kiasi, jambo linalosaidia kudumu muda mrefu baada ya kuvunwa.

Kiwango cha mafuta ni cha kati ya asilimia 5 hadi 12, na ladha yake ni laini na isiyo na tindikali, hivyo kufaa kwa watoto na wazee.
Bacon ni aina yenye matunda ya ukubwa wa wastani, uzito wake ukiwa kati ya gramu 250 hadi 350. Ngozi yake ni laini, yenye rangi ya kijani kibichi na umbo la duara-yai.

Ina kiwango cha mafuta cha asilimia 16 hadi 18 na hupendwa kwa kuwa rahisi kumenya na ina muda mzuri wa kuhifadhiwa.
Aina hii inalimwa zaidi katika maeneo yenye hali ya hewa ya wastani hadi baridi.
Ettinger ni parachichi lenye umbo kama la matunda ya mpera huku likitawaliwa na ngozi nyembamba na rangi ya kijani kibichi.
Uzito wake ni kati ya gramu 250 hadi 350, na kiwango cha mafuta ni asilimia 18 hadi 22.
Hii ni aina inayotambulika kwa ladha nyororo na uwezo wa kukomaa mapema, hivyo ni chaguo bora kwa wakulima wanaolenga masoko ya mapema kabla ya msimu wa mavuno makubwa kuanza.

Mikoa inyozalisha kwa wingi zao hili la parachichi kwa Tanzania ni Kagera, Kigoma, Rukwa, Tanga, Manyara, Iringa, Mara na Ruvuma.
Baada ya kufahamu aina za parachichi zinazopatikana na kulimwa kwa wingi Tanzania tukutane katika makal ijayo ambapo tutaangazia faida za kutumia tunda hilo kiafya.