Fahamu faida za unywaji wa kahawa

Na Lucy Samson
19 Aug 2025
Kahawa ni miongoni mwa vinywaji maarufu duniani huku kikiwa na historia pana inayorithishwa enzi na enzi. Bodi ya Kahawa Tanzania ( TCB), inabainisha kuwa Tanzania  inazalisha aina mbili za kahawa ambazo ni Arabika pamoja na Robusta zinazochangia wastani wa asilimia 60.9  na 39.1 ya uzalishaji wa kahawa nchini hatua inayotajwa kuchangia ongezeko la wanywaji wa […]
article
  • Ni pamoja na kuimarisha afya ya ubongo pamoja na kuimarisha utendaji kazi wa mwili na akili.

Kahawa ni miongoni mwa vinywaji maarufu duniani huku kikiwa na historia pana inayorithishwa enzi na enzi.

Bodi ya Kahawa Tanzania ( TCB), inabainisha kuwa Tanzania  inazalisha aina mbili za kahawa ambazo ni Arabika pamoja na Robusta zinazochangia wastani wa asilimia 60.9  na 39.1 ya uzalishaji wa kahawa nchini hatua inayotajwa kuchangia ongezeko la wanywaji wa kinywaji hicho.

Licha ya umaaarufu wake kinywaji hiki kina faida nyingi katika afya ya mwanadamu ikiwa kikitumiwa kwa usahihi katika vipimo vinavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Dk Zakia Hitami kutoka Chuo cha Afya ya Cam kilichopo jijini Dar es Salaam anasema kuwa unywaji wa kahawa kwa kiwango kinachoshauriwa husaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kisukari.

“Kunywa vikombe viwili hadi vitano vya kahawa kwa siku kunapunguza hatari ya kifo, lakini pia magonjwa ya moyo, kisukari na mishipa pamoja na kupunguza uwezo wa kupata aina fulani za saratani,”amesema Dk Hitami.

Husaidia kuimarisha afya ya ubongo

Kwa mujibu wa tovuti ya hospitali ya continental ya nchini India inabainisha kuwa unywaji wa kahawa unaweza kuboresha vipengele mbalimbali vya utendaji wa ubongo, ikiwa ni pamoja na kumbukumbu, hisia, uangalifu, viwango vya nishati na utendaji wa jumla wa utambuzi. 

Pamoja na hayo kahawa ina uwezo wa kudhibiti magonjwa ya uharibifu wa neva, yakiwemo ugonjwa wa ‘Alzheimer’ na ‘Parkinson’ pamoja na kupoteza kumbukumbu.

“Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa unywaji wa kahawa kwa kiwango cha wastani unaweza kuhusishwa na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kupoteza  kumbukumbu (dementia) na matatizo ya uwezo wa kiakili,” imesema tovuti ya masuala ya afya ya Healthline.

Matumizi ya kahawa pamoja na limao huongeza kasi ya kuchoma mafuta hivyokusaidia kupunguza uzito.Picha?Good House Keeping.

Husaidia kupunguza uzito

Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa kahawa huchangia katika kuyeyusha mafuta mwilini na hivyo kumsaidia mtumiaji wa kinywaji hicho kukabili tatizo la uzito mkubwa.

“Kahawa inaweza kusaidia kupunguza uzito, lakini matokeo yanaweza kutegemea sababu mbalimbali za mtu binafsi kama vile aina ya mlo anaokula, kiwango cha shughuli za mwili, au mwitikio wa mwili wake kwa kafeini.” imeeleza tovuti ya healthline.

Ili kupata matokeo mazuri unaweza kuchanganya vijiko kadhaa vya maji ya limao na mdalasini katika kikombe cha kahawa na ukatumia angalau mara mbili kwa siku.

Kupunguza hatari ya magonjwa ya muda mrefu 

Unywaji wa kahawa wa wastani umehusishwa na kupunguza hatari ya magonjwa kadhaa sugu ikiwemo aina ya pili ya kisukari kwa mujibu ya utafiti uliochapishwa na Shirika la Utangazaji BBC, 

Hii inaweza kuwa kutokana na antioxidants katika kahawa, ambayo hupunguza kuvimba na kulinda seli kutokana na uharibifu. 

Kuimarisha afya ya akili na mwili

Kahawa pia inatajwa kama chanzo cha kuchangamsha mwili wakati wa uchovu huku ikiweka sawa akili (activeness) kwa muda mrefu zaidi.

Tovuti ya health essential inabainisha kuwa kafeini huzuia athari za adenosini, ambayo ni kemikali ya ubongo inayochochea  hisia za uchovu hiyo kutoa msukumo wa nguvu unaosaidia kuondoa usingizi.

Athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa mfano miligramu 300  za kafeini zinaweza kuboresha umakini wa mwili na akili kwa kiasi kikubwa wakati wa mchana hata kwa watu ambao hawajalala vya kutosha

Pamoja na faida hizo ni muhimu kutumia kahawa kwa kiasi ili kudhibiti uraibu na matatizo mengine ikiwemo ya moyo na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa