Matunda ni sehemu muhimu ya lishe, yakiwawezesha makundi mbalimbali ya watu kuimarisha afya zao kupitia vitamini, madini na nyuzi lishe zinazostawisha mwili.
Ili kupata faida hizo, wataalamu wa afya hushauri kuosha matunda kwa maji safi, kumenya na kuyala kwa viwango vinavyotakiwa, lakini je unafahamu kuwa hata maganda ya matunda yanafaida mwilini?
Pendo Majengo, Afisa Lishe kutoka mkoani Tanga ameiambia Nukta Habari kuwa maganda ya matunda husaidia katika mchakato wa mmeng’enyo wa chakula kutokana na makapi mlo yanayopatikana humo.
“Maganda ya matunda yanakuwa na kiwango kikubwa cha kalsiamu pamoja na makapi mlo ambayo ni muhimu sana katika afya ya utumbo na mchakato wa mmeng’enyo wa chakula,” anasema Pendo.
Hurahisisha umeng’enyaji wa chakula tumboni
Maganda ya matunda huwa na utajiri wa nyuzi nyuzi ambazo kwa pamoja hurahisisha mchakato wa umengenyaji wa chakula tumboni pamoja na makapi mlo yanayosaidia mtu kuchakata vizuri chakula na kutoa uchafu mwilini.
“Kwa mfano maganda ya matunda kama chungwa (ganda jeupe linalobaki baada ya kumenya ganda la njano) yana kiwango cha kalsiumu mara sita zaidi ya kula tunda lenyewe bila ganda lake,” anasema Pendo.
Huulinda mwili dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa
Tovuti ya afya ya Helthline inabainisha kuwa maganda ya matunda yana kiwango kikubwa cha vioksisdishaji na flavonoidi zinazopunguza hatari ya magonjwa sugu yasiyoambukiza sugu saratani, kisukari na magonjwa ya moyo.
“Kazi kuu ya ‘antioxidants’ ni kupambana na molekuli zisizo thabiti zinazoitwa radikali huru, kiwango kikubwa cha radikali huru kinaweza kusababisha msongo wa oksidishaji (oxidative stress), hali ambayo huharibu seli na kuongeza hatari ya magonjwa. Watafiti wanaamini kuwa antioxidants husaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na baadhi ya aina za saratani,” imesema tovuti ya Healthline.
Husaidia kupunguza uzito
Baadhi ya maganda ya matunda husaidia mtu kushiba haraka na kukaa muda mrefu tumboni bila kuhitaji chakula cha ziada jambo linaloweza kusaidia kupunguza uzito.
“Vyakula vyenye nyuzi nyingi husaidia kupunguza kasi ya utumbo, kuongeza ujazo wa chakula tumboni, na kuhamasisha utengenezaji wa homoni zinazohusiana na hisia ya kushiba, kama vile cholecystokinin (CCK). Hii inasaidia kupunguza ulaji wa chakula na kudhibiti uzito,” inasema Tovuti ya masuala ya afya ya Harvard.
Aidha, mtaalamu huyo wa lishe anatoa ushauri na angalizo kwa jamii kuosha maganda hayo kwa maji safi na salama kabla ya kutumia ili kuua vijidudu pamoja na madawa yaliyotumika shamabani ambayo yanaweza kusababisha magonjwa.
Pamoja na hayo Pendo anasema maganda ya matunda pekee hayatoshi ni lazima kula pamoja na kiwango stahiki cha matunda na kula makundi yote sita ya vyakula ili kupata virutubisho zaidi.