Mafuta ya nazi ni miongoni mwa mafuta ya asili yanayotumika sana katika shughuli mbalimbali ikiwemo urembo wa ngozi na nywele.
Umaarufu wa mafuta haya ya asili yanayotokana na nazi ambazo hupitia michakato tofauti hadi kutumiwa kwa ajili ya urembo au maandalizi ya chakula.
Ndio! Mbali na kutumiwa katika urembo mafuta hayo yanaweza pia kutumika kupikia, kuoka au kukaanga aina mbalimbali za vyakula.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa matumizi ya mafuta haya katika mapishi huwa na faida nyingi za kiafya ikiwemo kuimarisha afya ya moyo.
“Lauric Acid’ iliyomo kwenye mafuta ya nazi inasaidia kudhibiti kiwango cha kolesteroli kwa kuongeza kolesteroli nzuri (HDL) na kupunguza ile mbaya (LDL). Matokeo yake ni moyo wenye afya, mzunguko mzuri wa damu na mwili wenye furaha zaidi…
… Ukiyatumia kwa kiasi, mafuta haya yanaweza kuwa mbadala mzuri wa baadhi ya mafuta yaliyosindikwa kupita kiasi,” amesema Devotha Mushumbusi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC).
Pamoja na faida hizo Mushumbusi ameongeza kuwa mafuta haya yakitumika kwa kiasi husaidia kuboresha mmeng’enyo wa chakula na kuchochea uchakataji wa nishati (energy breakdown), jambo linalosaidia kuupa mwili nguvu na kuongeza ufanisi wa mifumo ya mwili kufanya kazi kwa usahihi.
“Kwa mtu anayetaka kupunguza uzito, mafuta haya ni msaada mzuri kwani husaidia kupunguza hamu ya kula. Pia huchangia kuchoma kolesteroli na kusaidia mwili katika mchakato wa kupungua uzito,” ameongeza Mushumbusi.
Mafuta ya nazi yanaweza kutumika kwa njia mbalimbali jikoni. Unaweza kuyatumia kukaanga samaki, viazi, au vitafunwa kwa ladha ya kipekee ya kitropiki.
Pia, kuongeza kijiko kimoja cha mafuta haya kwenye mboga za majani au wali huboresha harufu na ladha yake.
Kadhalika, ukichanganya kiasi kidogo cha mafuta ya nazi kwenye keki au maandazi hupata ladha tamu na ya asili inayovutia zaidi.
Mafuta ya nazi si tu kwamba yanaboresha ladha ya mapishi yako, bali pia yanalinda afya ya moyo, kusaidia kupunguza uzito, na kuupa mwili nguvu.
Kwa hivyo, kuyatumia kwa kiasi na kwa utaratibu ni njia bora ya kufurahia ladha na afya kwa pamoja jikoni mwako.