Jinsi ya kutengeneza juisi ya nanasi na tango

Na Fatuma Hussein
14 Aug 2025
Ukiachana na ladha ya kinywaji hiki kinachofurahisha koo hutumiwa pia kuondoa sumu mwilini (detox).
article
  • Chanzo cha vitamini C, A na madini muhimu kwa afya.
  • Hutumiwa kama moja ya kinywaji cha kusaidia kuondoa sumu mwilini (detox).

Je unajua kama mchanganyiko wa nanasi na tango huweza kutengeneza juisi tamu na yenye faida nyingi mwilini?

Ukiachana na ladha ya kinywaji hiki kinachofurahisha koo, hasa katika siku za joto pia hutumiwa kama moja ya kinywaji cha kusaidia kuondoa sumu mwilini (detox).

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) matunda haya hususani nanasi lina virutubisho mbalimbali ikiwemo makapimlo, vitamini C, vitamini A, kirutubisho cha vitamini B kinachoongeza damu, potasiamu, kemikali za mimea na sukari ambavyo ni muhimu katika afya ya binadamu.

Jarida la masuala ya afya la healthline linabainisha kuwa tango lina faida nyingi kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kupunguza uzito na vitambi, kuthibiti wingi wa sukari mwilini na kukosa choo.

Fuatana nasi leo ndani ya JikoPoint.co.tz uweze kujua namna ya kuandaa juisi hii ili kupata faida zake.

Mahitaji

Nanasi 1 kubwa

Matango 2 saizi ya kati

Ndimu/limao 1

Majani ya mnanaa

Sukari (hiari sio lazima)

Baada ya kumalizia kuandaa juisi hii unaweza kuongeza majani machache ya mnanaa juu kama mapambo na kuongeza harufu ya kupendeza.picha/Juices.

Hatua kwa hatua namna ya kuandaa

Hatua ya kwanza, anza kwa kuandaa viungo vyako. Osha nanasi kisha menya kwa kuondoa maganda yake ya nje pamoja na sehemu ngumu nyeusi zilizopo ndani yake, kisha likate vipande vidogo.

Baada ya hapo osha tango kwa maji safi ya uvuguvugu ili kuondoa uchafu wowote na viuatilifu vilivyoweza kubaki, kisha likate vipande vidogo bila kumenya maganda yake, kwani ngozi ya tango ina virutubisho vingi na nyuzi asilia zinazosaidia mmeng’enyo.

Hatua inayofuata menya ndimu au limau, kisha likate vipande ili kurahisisha kuchanganya ladha yake na matunda mengine.

Hatua nyingine inayofuata baada ya viungo vyote kuandaliwa, weka vipande vya nanasi, tango na ndimu kwenye blender au juicer.

Ikiwa unatumia blenda unaweza kuongeza kiasi kidogo cha maji safi kusaidia kusagika vizuri kwa matunda.

Anza kusaga taratibu mchanganyiko wako, kisha ongeza kasi hadi viungo vyote vichanganyike vizuri na kuunda mchanganyiko laini dakika tano tu zinatosha kukamilisha zoezi la kusaga.

Ikiwa unatumia juicer, unaweza kuweka viungo moja kwa moja bila kuondoa sehemu ya katikati ya nanasi au kumenya tango, kwani mashine itachuja nyuzi na kutoa juisi safi moja kwa moja. Kama hupendi juisi yenye nyuzi nyingi, unaweza kuichuja ili kupata kinywaji laini zaidi.

Tumia chujio laini au kitambaa safi, kisha mimina mchanganyiko taratibu huku ukikandamiza ili kutoa juisi yote.Mpaka kufikia hapo unaweza mimina juisi yako kwenye glasi safi na uongeze barafu ili kuifanya iwe baridi na ya kustarehesha zaidi, hasa katika siku za joto.

Unaweza pia kuongeza majani machache ya mnanaa juu kama mapambo na kuongeza harufu ya kupendeza. Kinywaji hiki ni bora zaidi kinapotumika mara moja baada ya kutengenezwa.Ikiwa utabaki na juisi, iweke kwenye chupa

yenye mfuniko na kuihifadhi kwenye jokofu kwa muda usiozidi siku tatu hadi nne ili kudumisha ubichi na ladha yake asilia

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa