Spirulina: Hazina ya maji inayoboresha afya za Watanzania

Na Fatuma Hussein
17 Jul 2026
Kisayansi spirulina ni aina bakteria wa kijani-bluu (cyanobacteria),wenye uwezo wa kutengeneza chakula chao kupitia mwanga wa jua kama mimea.
article
  • Ni mwani mdogo usioonekana kwa macho kirahisi, lakini wenye virutubisho vingi.
  • Unatajwa kuwa miongoni mwa vyakula vya baadaye duniani.

Ni mwani mdogo usioonekana kwa macho kirahisi, lakini wenye virutubisho vingi.

Unatajwa kuwa miongoni mwa vyakula vya baadaye duniani. 

Dar es Salaam. Katika maji yenye chumvi nyingi ambayo kwa wengi huonekana hayafai kwa maisha ya kawaida, kuna mmea mdogo unao kuwa kimya kimya lakini wenye thamani kubwa kuliko wengi wanavyodhani. 

Mmea huo tunaouzungumzia katika makala hii unaitwa Spirulina ambao umejizolea umaarufu kutokana na utajiri wake mkubwa wa virutubisho.

Kwa miongo kadhaa, wanasayansi duniani wamekuwa wakiuita chakula cha baadaye kutokana na kiwango chake kikubwa cha protini, vitamini na madini muhimu kwa mwili wa binadamu. 

Wakati mataifa mengi yakitumia fedha nyingi kuuzalisha kwa teknolojia ya kisasa, Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira ya asili yanayoweza kuukuza.

Lakini je, Watanzania wengi wanaijua spirulina? Inapatikana wapi? Na kwa nini wataalamu wanaamini inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za lishe na uchumi?

Spirulina ni nini hasa?

Kisayansi spirulina ni aina bakteria wa kijani-bluu (cyanobacteria),wenye uwezo wa kutengeneza chakula chao kupitia mwanga wa jua kama mimea.

Kinachoufanya kuwa wa kipekee ni kiwango chake kikubwa cha virutubisho. Kwa uzito mkavu, zaidi ya asilimia 60 ya spirulina ni protini, jambo linaloufanya kuwa miongoni mwa vyakula vyenye protini nyingi zaidi duniani.

Pia una vitamini mbalimbali, madini ya chuma, magnesiamu, potasiamu na kemikali asilia zinazosaidia kulinda seli za mwili dhidi ya uharibifu.

Spirulina imeendelea kuvutia watafiti kutokana na mchango wake katika lishe na usalama wa chakula duniani. Picha |Canva.

Spirulina hupatikana wapi Tanzania?

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania, spirulina hukua katika maziwa yenye maji ya alkali na chumvi nyingi, mazingira ambayo si rahisi kwa viumbe wengi kuishi.

Utafiti uliofanywa na taasisi hiyo katika maziwa maarufu ya Bonde la Ufa yakiwemo Ziwa Natron, Ziwa Manyara, Big Momela na Small Momela yaliyopo mkoani Arusha ulibaini kuwa Tanzania ina mazingira rafiki ya uzalishaji wa mmea huo.

Maziwa haya yana kiwango kikubwa cha madini na hali ya alkali inayowezesha spirulina kustawi kwa wingi. 

Ndiyo maana maeneo hayo yamekuwa kivutio cha watafiti kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaochunguza uwezo wake katika lishe, afya na hata uchumi wa viumbe hai.

Spirulina inaweza kuchanganywa kwenye juisi, uji, mtindi au maziwa kama sehemu ya lishe bora. Picha | Canva.

Kwa nini spirulina imepewa hadhi ya “superfood”?

Umaarufu wa spirulina unatokana na faida zake nyingi kiafya ambazo zimeendelea kuchunguzwa na kuthibitishwa katika tafiti mbalimbali. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), virutubisho vilivyopo kwenye spirulina ikiwemo madini ya chuma, vitamini na viambata vinasaidia kulinda mwili dhidi ya uharibifu wa seli. 

FAO inaeleza kuwa spirulina inaweza kuchangia kuimarisha lishe na usalama wa chakula, hasa katika maeneo yenye upungufu wa virutubisho.

Ushahidi mwingine umetolewa na uchambuzi wa tafiti 12 za kitabibu (systematic review and meta-analysis) uliochapishwa mwaka 2019 katika jarida la Phytotherapy Research. 

Watafiti walibaini kuwa matumizi ya spirulina yalihusishwa na kupungua kwa kiwango cha sukari ya kufunga na kuboresha baadhi ya viashiria vya kimetaboliki kwa watu wenye kisukari au matatizo yanayohusiana na mfumo wa mmeng’enyo wa sukari. 

Unga wa spirulina, kirutubisho cha lishe kinachotokana na mwani wa kijani-kibluu unaopatikana katika mazingira yenye maji ya alkali na chumvi nyingi. Picha| Canva.

Hata hivyo, watafiti wanasisitiza kuwa spirulina ni kirutubisho cha lishe, si dawa ya kutibu magonjwa, hivyo matumizi yake yanapaswa kuwa sehemu ya lishe bora na si mbadala wa matibabu ya kitabibu.

Spirulina hutumikaje?

Baada ya kuvunwa na kusafishwa, spirulina hukaushwa na kusindikwa kuwa unga, vidonge au kapsuli.

Unga wake unaweza kuchanganywa kwenye juisi, maziwa, mtindi, uji au hata kuongezwa kwenye vyakula mbalimbali bila kupoteza virutubisho vyake vingi.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa matumizi yake yafuate kiwango kinachoshauriwa na wataalamu wa afya au maelekezo ya bidhaa husika.

Spirulina husindikwa na kupatikana katika mfumo wa unga, vidonge au kapsuli, na hutumika kama kirutubisho cha lishe kutokana na wingi wa protini na virutubisho vingine. Picha| Canva.

Licha ya kuwa na mazingira yanayoruhusu ukuaji wa spirulina, uzalishaji wake nchini bado uko katika kiwango kidogo ukilinganishwa na mahitaji ya soko la dunia.

Mbali na kuboresha lishe ya wananchi, sekta hiyo inaweza kufungua ajira kwa vijana, kuongeza mapato ya wakulima na kukuza mauzo ya bidhaa zenye thamani kubwa katika soko la kimataifa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa