TBS: Mbogamboga hazina mabaki ya sumu, viuatilifu

Na Lucy Samson
30 Sept 2025
TBS imesema imechunguza aina mbalimbali za mbogamboga na kubani kuwa hazina mabaki  ya viwatilifu kama ilivyoripotiwa hivi karibuni.
article
  • Ni baada ya kufanya uchunguzi katika masoko yanayouza mbogamboga nchini.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema limechunguza aina mbalimbali za mbogamboga na kubani kuwa hazina mabaki  ya sumu na viwatilifu kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni.

Septemba 28, 2025 gazeti la Mwananchi liliripoti tabia ya baadhi ya wakulima kuvuna mbogamboga ikiwemo nyanya siku chache baada  ya kupuliza dawa ili zisiharibike jambo lililotajwa kuhatarisha afya za walaji.

Taarifa ya Gladness Kaseka, Meneja wa Uhusiano na Masoko wa TBS iliyotolewa jana Septemba 29, 2025 inafafanua kuwa mbogamboga hizo zina kiwango himilivu cha viwatilifu hivyo ni salama kwa walaji.

“Ufuatiliaji na uchunguzi wa kimaabara wa aina mbalimbali za mbogamboga katika soko umeonesha kuwa mazao hayo hayana mabaki ya viuatilifu (pesticide residues) yanayozidi kiasi kinachovumilika (maximum residue limit) kwa mujibu wa viwango vya WHO/FAO,” imesema taarifa ya Kaseka.

Kilimo cha mazao ya mbogamboga  hutumia viuatilifu ili kukabiliana na wadudu waharibifu, magonjwa ya mimea na magugu ambapo viuatilifu vinavyotakiwa kutumika ni vile vilivyoidhinishwa na mamlaka za udhibiti.

Ili kupunguza matumizi makubwa ya viwatilifu wakulima wa mbogamboga hushauriwa kulima kisasa kwa kutumia ‘screen house’ au ‘green house’.Picha/Lucy Samson.

Pamoja na viuatilifu hivyo kuidhinishwa na mamlaka za udhibiti bado mkulima anatakiwa kuvitumia kwa kiwango stahiki ili kupunguza uwezekano wa viwatilifu hivyo kuingia katika mwili wa binadamu wakati wa kula.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) viuatilifu vinaweza kusababisha madhara ya haraka au ya muda mrefu (chronic), kulingana na kiwango na namna mtu alivyoathiriwa nazo.

“Mabaki ya viuatilifu  yanaweza kusababisha sumu ya haraka (acute poisoning) au madhara ya muda mrefu ya kiafya, yakiwemo saratani na matatizo ya uzazi,” imesema WHO.

Mbali na walaji wa mboga mboga zilizokuzwa kwa viuatilifu WHO imetahadharisha makundi mengine ya watu ikiwemo wakulima mashambani na bustanini kuwa makini wakati wakizitumia ili kujilinda na mdhara ya kiafya.

Aidha, TBS imesema itaendelea kufanya ufuatiliaji wa bidhaa za mbogamboga na kushirikiana na mamlaka inayohusika na udhibiti wa afya ya mimea na viuatilifu ili kuhakikisha usalama wa mbogamboga unazingatiwa na wadau wote katika mnyororo wa thamani.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa