Mlonge ni mmea wa asili unaopatikana maeneo ya tropiki duniani, hasa Afrika Mashariki, India na Asia Kusini.
Mmea huu unaojulikana kitaalamu kama Moringa oleifera umekuwa ukitumika katika tiba asilia na lishe kutokana na uwezo wake wa kipekee wa kutoa virutubishi na kutibu magonjwa mbalimbali.
Mmea huu pia unajulikana kama ‘mti wa miujiza’ kutokana na kusheheni virutubishi vingi ikiwemo vitamini A, B, C na E pamoja na madini kama kalsiamu, chuma, potasiamu na magnesiamu.
Aidha, mlonge una sifa ya kuwa na vioksidishaji (antioxidants) vinavyosaidia kupambana na sumu mwilini na kuimarisha kinga ya mwili.
Kwa karne nyingi, watu wa jamii za kale wamekuwa wakitumia kila sehemu ya mti huu kuanzia majani, mizizi, mbegu, maua, na magome kama chakula, dawa, au kiungo cha kusafisha maji.
Kwa mujibu wa tovuti ya Medical News Today uwezo wa mlonge kukua haraka, kustahimili ukame na kuwa na gharama ndogo ya kuzalishwa, umeufanya kuwa moja ya mimea inayopendekezwa sana kwa kupambana na utapiamlo na magonjwa yanayotokana na lishe duni, hasa katika nchi zinazoendelea.
Baada ya kuufahamu vyema mmea huu Jikopoint.co.tz imekusogezea faida na matumizi ya mlonge ambao ni muhimu katika afya ya binadamu.
Pendo Majengo Afisa Lishe kutoka mkoani Tanga katika mahojiano na Jikopoint, amebainisha kuwa, mbegu za mlonge zina faida nyingi ikiwemo uwepo wa madini ya zinki ambayo ni muhimu katika mfumo wa uzazi.
“Mbegu hizi zina mafuta bora yenye virutubisho na madini kama zinki, ambayo yana mchango mkubwa katika afya ya mfumo wa uzazi na usawa wa homoni kwa ujumla,” ameeleza Majengo
Mlonge umethibitishwa kuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia kudhibiti ugonjwa wa kisukari, hasa aina ya pili (Type 2 diabetes).
Uwezo huu unatokana na uwepo wa kampaundi aina ya ‘isothiocyanates’, ambazo husaidia kuimarisha utoaji wa insulini na kuzuia kushuka au kupanda kwa viwango vya sukari katika damu.
Tovuti ya National Library of Medicine inaeleza kuwa tafiti za awali zilizofanyika kwa wanyama na binadamu wachache zimeonesha kuwa unga wa majani ya mlonge unapopatikana kwa kiasi sahihi, unaweza kusaidia kudhibiti viwango vya sukari baada ya mlo kwa watu wanaougua kisukari
Aidha, pamoja na kusaidia udhibiti wa sukari, tovuti ya masuala ya afya ya Healthline inaeleza kuwa mlonge una uwezo wa kupunguza hatari ya matatizo ya kiafya yanayotokana na kisukari, kama vile uharibifu wa mishipa midogo ya damu, ini na figo.
Kampaundi zilizopo ndani yake huchochea matumizi bora ya glukosi na kupunguza uvimbe ndani ya mwili, hali inayosaidia kudhibiti kisukari kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo, watafiti wanaendelea kuchunguza madhara na manufaa yake kwa matumizi ya muda mrefu
Tovuti ya Healthline inafafanua kuwa mlonge pia husaidia kudhibiti shinikizo la damu, tatizo ambalo linahusishwa na maradhi ya moyo na kiharusi.
Kampaundi aina ya ‘quercetin’ inayopatikana kwa wingi kwenye majani ya mlonge husaidia kupunguza msongamano wa mishipa ya damu, kwa kupunguza viwango vya oksidi ya nitriki na kuimarisha mzunguko wa damu. Hii hufanikisha kupungua kwa presha ya damu mwilini.
Zaidi ya hayo pia mlonge hutoa kinga dhidi ya mabadiliko mabaya katika mishipa ya damu yanayosababishwa na lehemu nyingi (cholesterol).
Kwa kusaidia kushusha kiwango cha mafuta mabaya mwilini, mlonge husaidia kuzuia kukakamaa kwa mishipa ya damu, hali inayochangia maradhi sugu ya moyo.
Hata hivyo, tovuti ya National Library of Medicine (NHI) inaeleza kuwa mlonge unatajwa kuwa tiba ya asili ya magonjwa yanayohusiana na mzunguko wa damu.
Kulingana na tovuti ya NHI mlonge unatajwa kuwa na uwezo wa kuzuia au kuchelewesha ukuaji wa chembe chembe za saratani.
Hili linawezekana kutokana na uwepo wa ‘niazimicin’ na ‘glucosinolates’, kampaundi zenye uwezo wa kuua chembe zisizo za kawaida zinazohusiana na saratani, hasa saratani ya tezi dume, matiti, ini na koloni.
Aidha, kampaundi hizi huongeza kinga ya mwili kwa kupunguza uvimbe na uharibifu wa DNA unaochochewa na kemikali hatari.
Wataalamu wa tiba asilia wanashauri matumizi ya mlonge kama nyongeza ya tiba, hasa kwa wagonjwa wanaopambana na mabadiliko ya chembe mwilini.
Hata hivyo, haipaswi kuwa mbadala wa tiba rasmi bali kiungo kinachosaidia mchakato wa uponyaji
Majani ya mlonge ni chanzo bora cha vioksidishaji (antioxidants) kama vitamini A, C, E na polyphenols ambazo huongeza kinga ya mwili na kusaidia mwili kupambana na magonjwa ya kuambukiza.
Vioksidishaji hivi hupambana na sumu za oksijeni (free radicals) ambazo hushambulia seli na kusababisha magonjwa kama kisukari, saratani, na magonjwa ya moyo.
Pia, mlonge una madini muhimu kama kalsiamu, chuma na potasiamu ambayo husaidia kuimarisha mifupa, misuli, na viungo muhimu.
Kwa watu wanaokosa virutubisho kutokana na lishe duni au mazingira ya maisha, mlonge husaidia kurejesha hali ya afya na kuongeza nguvu mwilini.
Hii ndiyo sababu unaendelea kupendekezwa kama sehemu ya lishe ya kila siku.
Mlonge hupunguza hamu ya kula na kuchochea uchomaji wa mafuta mwilini. Hii husaidia watu wenye uzito mkubwa kupunguza kilo kwa njia salama.
Aidha, hupunguza kiwango cha sukari na mafuta katika damu, hali inayosaidia kudhibiti uzito na lishe bora.
Kwa kuwa na nyuzinyuzi (fiber), mlonge husaidia mmeng’enyo mzuri wa chakula. Hupunguza matatizo kama kuvimbiwa, gesi na tumbo kujaa.
Mlonge pia husaidia kusawazisha bakteria wazuri ndani ya utumbo mdogo, hali inayoboresha afya ya mfumo wa chakula kwa ujumla.
Mafuta ya mlonge hutumika katika vipodozi kutokana na uwezo wake wa kulainisha na kurekebisha ngozi.
Hupunguza mba, chunusi na uzee wa ngozi.
Kwa nywele, mafuta ya mlonge huimarisha mizizi, kuzuia kukatika na kusaidia ukuaji wa nywele kwa haraka.
Kulingana na tovuti ya Uly Clinic Majani ya mlonge hutumika kutibu homa ya matumbo (typhoid) kwa njia ya asili.
Kampaundi zilizo ndani yake huua vimelea wa bakteria wanaosababisha homa hiyo.
Kwa wagonjwa wa typhoid, juisi ya majani mabichi au unga wa majani unaweza kusaidia kupunguza dalili kwa haraka.
Hata hivyo, matumizi haya yafanyike kwa ushauri wa kitaalamu.
Kwa kuzingatia maelezo haya, hakuna shaka kuwa mlonge ni miongoni mwa mimea yenye thamani kubwa kiafya katika kizazi cha sasa na kijacho.