Biashara kati ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepaa kwa asilimia 8.9 ndani ya mwaka mmoja ikichangiwa na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara nchini.
Jumuiya hiyo inayoundwa na nchi nane zilizopo mashariki mwa bara la Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudani ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni miongoni mwa masoko muhimu ya kikanda yanayochochea ukuaji wa sekta ya biashara nchini.
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake leo Mei 22, 2026 bungeni Dodoma amesema ongezeko hilo limetokana juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya biashara nchini.
“Ongezeko hilo limechangiwa na juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara nchini na kuimarika kwa uzalishaji wa bidhaa ambazo zina soko kubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Kapinga.
Mwaka 2025 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Sh 3.2 trilioni (Dola za Marekani bilioni 1.2) katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikilinganishwa na Sh3.0 trilioni (Dola za Marekani bilioni1.1) mwaka 2024.
Bidhaa zilizopaisha mapato hayo ni vitunguu, samaki, karanga, nyanya, asali, maharage, mbaazi, dagaa, mahindi, ngano, mchele, karatasi, mabati na vigae.
Hivi karibuni Rais Samia alikutana na baadhi ya marais wa EAC katika ziara za kikazi zilizofanyika nchini ambapo pamoja na mambo mengine wakuu hao wa nchi walijadiliana kuimarisha uchumi wa kikanda na kuondoa vikwazo vya biashara mipakani.
Miongoni mwao ni William Ruto, Rais wa Kenya ambaye pamoja na kujadili ushirikiano katika miradi ya kimkakati walikubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kikodi baina ya nchi hizo mbili ili kutoa fursa ya kukuza biashara na uwekezaji kwa pande zote.
“Kama mnavyojua dunia ya sasa ushirikiano kati ya mataifa umejikita zaidi kwenye mambo ya kiuchumi…tumewapa watendaji wetu muda mpaka mwisho wa mwezi Mei wawe wamemaliza vikwazo vyote vya kikodi,” amesema Rais Samia Mei 4, 2025 alipokuwa akizungumza na wanahabari baada ya Rais Ruto kuwasili kwa ziara ya kikazi nchini Tanzania.
Mbali na Ruto, Tanzania pia ilimpokea Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambao wote walikubaliana kuboresha mazingira ya biashara baina ya nchi hizo.
Pamoja na kuuza EAC, mwaka 2025Tanzania pia ilinunua bidhaa bidhaa zenye thamani ya Sh1.4 trilioni (Dola za Marekani milioni 563.1) kutoka nchi za EAC ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya Sh1.3 trilioni (Dola za Marekani milioni 527.3 mwaka 2024), sawa na ongezeko la asilimia 6.8.
Kwa mujibu wa Kapinga, ongezeko hilo limetokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani ikiwemo sabuni za kuogea, vifaa vya mitaji, vyakula vilivyosindikwa, misumari, dawa za viatu, maziwa na vifaa vya usafirishaji.