Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia Oktoba 2023 imepungua kwa asilimia moja ikichangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula ikiwemo ngano, mchele na nyama.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa Novemba 8, 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kasi ya mfumuko wa bei imepungua kutoka asilimia 3.3 iliyorekodiwa mwaka ulioishia Septemba 2023 hadi asilimia 3.2 kwa mwaka unaoishia mwezi Oktoba mwaka huu.
“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2023 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2023…” imeeleza taarifa ya NBS.
Kwa mujibu wa NBS, bidhaa hizo za chakula zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na ngano kutoka asilimia 3.1 hadi asilimia 2.4, mchele (kutoka asilimia 7.6 hadi asilimia 4.4), samaki wabichi (kutoka asilimia 8.0 hadi asilimia 7.1) na dagaa wakavu kutoka asilimia 13.5 hadi asilimia 11.0
Nyingine ni samaki wakavu kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 6.7, matunda (kutoka asilimia 10.4 hadi asilimia 6.1), mihogo mibichi (kutoka asilimia 7.4 hadi asilimia 7.1), magimbi (kutoka asilimia 13.6 hadi asilimia 11.3), maharage (kutoka asilimia 16.3 hadi asilimia 10.3), choroko kavu (kutoka asilimia 3.0 hadi asilimia 1.1) na njegere kavu kutoka asilimia 8.6 hadi asilimia 8.4.
Kushuka kwa bei ya bidhaa hizo kunaashiria unafuu kiduchu katika upatikanaji wa bidhaa kulinganisha na miezi mitatu iliyopita mabapo kiwango cha mfumuko wa bei kiling’ang’ania asilimia 3.3.
Aidha, NBS imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2023 nao umepungua hadi asilimia 4.5 kutoka asilimia 5.6 uliyorekodiwa mwaka ulioishia Septemba, 2023.
Kwa upande wa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Septemba, 2023 umeongezeka kidogo na kufikia asilimia 2.6 kutoka asilimia 2.4 iliyorekodiwa mwaka ulioishia Oktoba, 2023.