Jinsi ya kutengeneza dagaa nyama nyumbani

Na Mlelwa Kiwale
27 Aug 2024
Dagaa wa nyama au maarufu kama dagaa wa Zanzibar  ni mboga inayozidi kujizolea umaarufu katika masoko mengi nchini, wakisambaa kutoka mikoa ya Pwani kama Dar es Salaam, hadi mikoa isiyopitiwa na bahari ikiwemo Kilimanjaro na Arusha. Umaarufu wa dagaa hawa unatokana na uwezo wake wa kuhifadhiwa hadi miezi sita na kuwawezesha wafanyabiashara kuwasafirisha maeneo mbalimbali […]
article
  • Si kwa matumizi ya nyumbani tu bali hata kwa biashara dagaa hawa wanafaa.

Dagaa wa nyama au maarufu kama dagaa wa Zanzibar  ni mboga inayozidi kujizolea umaarufu katika masoko mengi nchini, wakisambaa kutoka mikoa ya Pwani kama Dar es Salaam, hadi mikoa isiyopitiwa na bahari ikiwemo Kilimanjaro na Arusha.

Umaarufu wa dagaa hawa unatokana na uwezo wake wa kuhifadhiwa hadi miezi sita na kuwawezesha wafanyabiashara kuwasafirisha maeneo mbalimbali nchini na kujipatia faida.

Lakini je? Unafahamu kuwa unaweza kuwandaa na kuwakausha dagaa nyumbani ili uweze kufaidi utamu wa mboga hiyo kwa muda mrefu?.

Ndiyo! Kwa wanaoishi kando ya bahari unaweza kununua dagaa hawa wakiwa wabichi na ukawaandaaa mwenyewe nyumbani kwa ajili ya kuwahifadhi kwa muda mrefu kwa mahitaji ya familia yako au kwa ajili ya biashara.

Utakachohitaji ni dagaa wabichi (kiasi chako),maji safi, chumvi na sehemu ya kuwaanika ikiwemo ungo, kiroba au wavu safi.

Jinsi ya kuandaa

Maandalizi ya njia hii ya kuhifadhi yataanza kwa kuwasafisha dagaa baada ya kuwanunua kwa wachuuzi au baharini, unaweza pia ukawatoa utumbo na kichwa ili wasioze wakiachwa kwa muda mrefu.

Baada ya kuondoa uchafu na kuosha utawachuja kwa muda wa dakika tatu kisha utawaekea chumvi na kuanza kuwapeta ili wachanganyike vizuri.

Hakikisha unaweka chumvi nyingi ya kutosha kwani ndiyo kiungo pekee kitakachowezesha dagaa kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.

Hatua inayofuata ni kuwasha jiko na kuwachemsha dagaa kwa moto wa wastani wa dakika 10 au zaidi ila hakikisha haukorogi kwa kutumia mwiko au kijiko na hawaivi kwa kupitiliza hadi kuwa uji uji.

Utaendelea na hatua hiyo hadi maji yatakavyoanza kukauka kisha utaenda kuwamiminia katika sehemu safi kama ungo, sahani kubwa au kiloba kilichokuwa kisafi.

Dagaa wakiiva watoe uwachuje maji yote yatoke kisha uwaanike juani ili wakakuke vizuri kabla ya kuwahifadhi au kuwasafirisha.

Ili kupata matokeo mazuri wageuze dagaa kila baada ya saa sita hadi saba ili wakauke vizuri kwa ukiridhishwa na kaukaji huo watakuwa tayari kwa kupikwa au kuhifadhi kwa zaidi ya miezi sita.

Dagaa wasipoweza kukauka vizuri hawataweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa