Dar es Salaam. Mwani ni miongoni mwa mimea tiba iliyojizolea umaarufu miaka ya hivi karibuni licha ya kuwepo kwa zaidi ya miongo kadhaa.
Mwani ambao pia hujulikana kwa jina la ‘Seamoss’ hukua na kumea baharini katika rangi mbalimbali ikiwemo kijani, nyeusi, zambarau, njano au nyekundu kama ilivyo kwa magugu mengine yanayoota baharini,
Zao hili ni chanzo cha virutubishi vingi vinavyohitajika katika mwili wa binadamu ikiwemo kalsiam, chuma, magnezium, zink na kopa kama inavyoelezwa katika tovuti ya Healthline.
Ikiwa wewe ni mtumiaji wa mwani au hujaanza kuutumia makala hii ni kwa ajili yako ambapo tutangazia faida za kiafya za mwani, aina zake na jinsi unavyoweza kuutumia nyumbani.
Tovuti ya healthline inasema matumizi ya mwani huweza kudhibiti kiwango cha Lehemu(cholesterol) kinachoingia mwilini ambacho mara nyingi kikizidi huziba mishipa ya damu hivyo kusababisha magonjwa ya moyo.
“Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya mwani hupunguza Lehemu (cholesterol) ambayo husaidia kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo,” imesema tovuti ya Healthline.
Mwani una nyuzi nyuzi nyingi za lishe, nyuzi hizo huyeyushwa vyema na bakteria waliopo kwenye utumbo hivyo kurahishsa mchakato wa ufyonzaji maji na kumuepusha mtumiaji kupata choo kigumu na magojwa kama bawasili na kansa ya utumbo.
Matumizi ya mwani huweza kuimarisha afya ya uzazi kwa mwanaume na mwanamke kutokana na uwepo wa madini ya zinki, madini chuma na kalsiam ambayo husaidia kudhibiti mfumo wa homoni na kuchangia uzalishaji wa mbegu za kiume kwa mwanaume.
Hata hivyo, tovuti ya Heathline imebainisha kuwa hakuna utafiti unaonyesha moja moja kuwa matumizi ya mwani yanaweza kumaliza kabisa matatizo ya uzazi hivyo imewataka watumiaji kuwa makini kutoitumia kupitiliza pia kutafuta ushauri wa daktari kabla ya matumizi.
Mbali na faida hizo, Aisha Nasir Mkurugenzi wa kampuni ya Africare inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za mwani anasema matumizi ya mwani huweza pia kusaidia watu wenye matatizo ya mgongo, magoti pamoja na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.
Matumizi ya mwani
Kwa mujibu wa Nasra matumizi ya bidhaa hiyo hutegemeana na mahitaji ya muhusika unaweza kuchagua kutumia mwani ya unga au jeli ambazo zote hufanya kazi aina moja mwilini.
“Kuna aina mbalimbali za mwani, kuna ya unga na jeli, na hapa kwenye jeli sisi tumeongeza na ladha ya matunda ili iwe rahisi kwa mtu kuitumia,” amesema Aisha.
Pia, tovuti ya Healthline inasema wapo watengenezaji ambao huitengeneza mwani katika mfumo wa vidonge, wengine huchanganya kwenye vinywwaji na bidhaa baridi kama ‘Ice cream’ ili iwe rahisi kwa wahitaji kutumia.
Kwa matumizi ya nyumbani unaweza kununua mwani wa unga ukachanganya kwenye maji ya moto ukatumia kama chai, ukaichanganya kwenye juisi au chakula wakati wa kuandaa.