Dar es Salaam. Waswahili walisema ‘kazi ni kazi ilimradi mkono uende kinywani’ wakimaanisha kwamba hakuna kazi ndogo au isiyo na thamani ilimradi inakupatia riziki ya kila siku.
Msemo huu wa waswahili unajidhihirisha kwa Abel Albert (22) muuza magimbi maarufu katika eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam anayefanya shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.
Tofauti na mitazamo ya watu kuhusu biashara hii Albert anasema magimbi yaanamuwezesha kumudu gharama za maisha na kumiliki vyanzo vingine vya mapato ikiwemo mashamba.
“Hii biashara inanisaidia kulipa kodi pia kuna vishughuli vidogo vidogo vya mkoani kwenye kulima vinanisaidia, kwenye mambo ya maradhi nimeugua ghafla inanisaidia pia na kwenye maswala ya mavazi inanisaida sana kwa kweli,” amesema Albert.
Albert anasema aliamua kufanya biashara hiyo kutokana na kuipenda pamoja na kugundua uhaba wa bidhaa hiyo katika soko la Mwananyamala ambapo Sh 50,000 ilitosha kabisa kuwa mtaji wa kuanzisha biashara hiyo.
Si Albert pekee anayenufaika na uuzaji magimbi, Christina John mmiliki wa mgahawa kutoka Mwananyamala sokoni ameiambia Nukta Habari kuwa uuzaji wa magimbi kama kitafunwa kumebadilisha mfumo mzima wa maisha yake.
“Namshukuru Mungu kwa kweli najipatia riziki mimi na familia yangu, maisha yangu pia yanaenda kupitia hiyo hiyo kazi kwa miaka miwili sasa,” amebainisha Christina.
Christina anasema aliamua kuuza magimbi katika mgahawa wake kutokana na uhitaji wa wateja wanaomzunguka katika eneo hilo.
“Magimbi ya kuchemsha ni chakula cha asili na watu wanakipenda kwahiyo nilivyochemsha siku ya kwanza watu waliyapenda, nikachemsha tena siku ya pili nikaona niendelee kwa kuwa ndio kitu watu wanakipenda,” ameongezea Christina.
Christina amebainisha kuwa kipande kimoja cha gimbi yeye huuza Sh 500, muhogo Sh 300 pamoja na viazi vitamu Sh 300 huku mchanganyiko wa magimbi na maharage unaoitwa ‘kivuge’ kwa kirugulu na ‘kishumba’ kwa kisambaa ambacho kinauzwa Sh 1,500 hadi Sh 2,000 kwa sahani.
Magimbi yanabana bajeti
Wakati wafanyabiashara wa magimbi wakitunisha mifuko yao kutokana na faida wanayoipata katika uuzaji wa chakula hicho, baadhi ya watu hukitumia kubana bajeti na kupunguza gharama ya kununua chakula kingine.
Miongoni mwa walaji hao yupo James James mkazi wa Mwananyamala sokoni ambaye hula magimbi kwa siku humsaidia kuepuka matumizi yasiyo ya lazima katika upande wa chakula.
“Magimbi ukinunua ya Sh 4,000 una uwezo wa kula milo mitatu ya siku nzima unakula asubuhi, unakula mchana na ukala na usiku…
…Ukitumia milo mingine asubuhi utatumia Sh 1,500 mchana Sh 2,000 na jioni utatumia Sh 2000 ina maana jumla itakuwa Sh 5,500 wakati ukinunua magimbi ya Sh 4,000 unatumia siku nzima, utakuwa ushaimaliza siku yako vizuri,” ameongezea James.
Naye Ramadhani John mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam anasema magimbi hukaa kwa muda mrefu tumboni na ni chakula kizuri kwa wanaofanya kazi ngumu ikiwemo za kubeba mizigo.
“Mimi huwa nakula magimbi asubuhi kwa sababu yananisaidia sana katika kazi zangu za kubeba mizigo kwa hiyo hapo siwazi tena kununua chakula mpaka jioni kuliko nikinunua chakula kingine huwa hakikai muda mwingi tumboni,” amesema John.
Bei, upatikanaji wa magimbi pasua kichwa kwa wafanyabiashara
Mfanyabiashara wa magimbi Agness Kawichi ameiambia Nukta Habari kuwa bei ya magimbi kwa sasa ipo juu, kulinganisha na vipindi vingine jambo linalominya faida wanayoingiza kwa siku.
Kawichi amebainisha kuwa bei ya magimbi kwa sasa imefikia Sh 80,000 kwa kiroba cha kilo 25 cha magimbi maole, magimbi maji Sh 100,000 hadi Sh 150,000 huku ujazo wake ukiwa mdogo kulinganisha na kipindi cha nyuma.
“Bei ya magimbi ipo juu vibaya mno na ukiangalia vile vile ujazo wake ni mdogo, biashara kwa ujumla kwa sasa ni ngumu sana na zamani wateja walikuwa wanapatikana wengi na magimbi yanapatikana kwa wingi ila kwa sasa hivi ukimwambia mteja aje kununua gimbi moja kama hilo Sh 2000 na anafamilia inakuwa ni ngumu…
…Kwahiyo haya sasa hivi yanatumika kwa watu aidha inakuwa mtu anampelekea mtoto au mgonjwa unakuta ununuaji wake tofauti na zamani,”amesema Kawichi.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamewashauri watu wengine wanaotaka kuanzisha biashara ya magimbi au yoyote ile kuwa wavumilivu kwasababu kila biashara ina changamoto zake.