“Kutumia gesi wakati wa kupika chakula kuna raha yake, kwanza chakula kinaiva haraka, kinakuwa kisafi na vyombo havichafuki,” anasema Halima Bakari, mama ntilie wa jijini Mwanza mwenye tamaa ya kutumia gesi kwenye kazi zake lakini hofu ya gharama inamrudisha nyuma.
Kulingana na hofu yake, Halima anabaki akinung’unika wakati wa mapishi yake kwani analazimika kutumia mkaa anaomini una bei nafuu.
Vumbi, majivu, moto mkali na kukosa uhakika wa ubora wa mkaa ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa mama ntilie huyu na maelfu ya Watanzania wengine.
Unapozungumzia nishati ya uhakika kwa ajili ya kupikia Watanzania, hauwezi kuacha kuutaja mkaa na kuni.
Watu wengi hutumia nishati hiyo kwa sababu ni rahisi kupatikana na wanaweza kumudu gharama yake tofauti na nishati nyingine kama umeme na gesi.
“Nishawahi kutumia gesi kipindi cha nyuma nilikuwa natumia mtungi mdogo na baada ya kuisha niliacha, si kwamba sipendi ila chakula cha mamantilie mara nyingi ni vema kutumia mkaa kwa kuwa tunahofia huenda gesi inaweza kuwa inatumika na kuisha haraka zaidi,” amesema Halima.
Ripoti ya Utafiti wa Upatikanaji na Matumizi ya Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2020, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) inaeleza kuwa, asilimia 63.5 ya kaya za Tanzania Bara wanatumia kuni kupikia ikifuatiwa na mkaa unaotumiwa na asilimia 26.2.
Hilo lina maanisha bado idadi kubwa ya kaya zinatumia kuni, mkaa na chache zinazotumia gesi, umeme na nishati zingine.
Licha ya sifa yake ya kupatikana kwa urahisi na watu kumudu gharama zake, mkaa na kuni vinatajwa kuwa hatari kwa mazingira na afya ikiwemo macho, kifua na saratani ya umio (oesophageal cancer).
Kama siyo mkaa, nini kinaweza kumfaa Halima?
Kinachoendelea katika maisha ya Halima, ni tofauti na baadhi ya wanawake mkoani Mwanza ambao wamechagua kutumia nishati safi na salama ya kupikia akiwemo Martha Kunju, Mkazi wa Usagara jijini humo.
Kunju yeye anatumia nishati ya gesi ya majumbani (PPG) kwa ajili ya kupikia. Anamiliki mtungi wa kilo 15 ambao hutumia kwa muda wa miezi minne na kwamba anapika kila aina ya chakula isipokuwa maharage na makande ambayo hulazimika kutumia jiko la mkaa kwa hofu ya gharama.
“Napikia vyakula vyote kuanzia chai hadi chakula cha mchana na jioni na ninatumia kwa muda wa miezi minne, mtungi huu huwa najaza kwa Sh54,000,” amesema Kunju.
Gharama ya Kunju ni sawa na gharama ya siku tano tu kwa Martha ambaye hununua mkaa wa Sh10,000 kila siku kukamilisha mapishi yake katia biashara ya mgawaha.
Endapo Martha atachagua gesi badala ya mkaa, atapunguza gharama za mafuta ya taa, viwashio na muda wa kusubiri jiko likolee na wakati huo kulinda afya yake.
Kwa upande wa maharage na makande, anachohitaji Martha na hata Kunju ni vifaa muhimu kwa ajili ya kuendelea kupika maharage na makande kwenye jiko lake la gesi.
Tofauti na wapishi wengine, wapishi wanaotumia nishati mbadala na safi wana nafuu zaidi na uhakika wa kuivisha chakula chao vizuri tena bila kuwa na harufu ya moshi.
Halima anasema, mpishi anayetumia gesi anatumia muda mfupi kupika hivyo huivisha haraka tofauti na anayetumia mkaa au kuni.
“Kwanza unapotumia mkaa unatumia muda mrefu zaidi hadi mkaa ushike ndipo uanze kupika tofauti na anayetumia gesi au umeme ambapo anatumia muda mfupi na chakula kinakuwa tayari,” amesema Halima.
Ni wakati sasa kwa wanawake ambao ndiyo waathirika wakubwa wa matumizi wa kuni na mkaa kugeukia nishati safi na salama kwa maendeleo endelevu.